Na Baltazar Mashaka, Mwanza

Banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika uwanja wa Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza, limeendelea kuvutia mamia ya wananchi wanaofika kujionea bunifu mbalimbali zinazotengenezwa na wanafunzi wa vyuo vya ufundi kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kuona bidhaa na teknolojia zilizobuniwa na vijana wanaopata mafunzo ya ufundi stadi, ikiwemo vifaa vya kilimo, bidhaa za viwandani, teknolojia za umeme, useremala, uchomeleaji, ushonaji na fani nyingine zinazolenga kutoa suluhisho la mahitaji ya jamii na soko la ajira.

Akizungumza leo, Bakari Athuman ambaye ni Mwalimu wa Uungaji vyuma wa VETA , alisema maonesho hayo yanatoa nafasi ya kuwaonesha wananchi mchango wa elimu ya ufundi stadi katika kuibua vipaji, kukuza ubunifu na kuwawezesha vijana kujiajiri badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee.

Aidha, wananchi wameeleza kufurahishwa na kiwango cha ubunifu kinachoonyeshwa na vijana hao, wakisema bidhaa nyingi zinazozalishwa zina ubora unaoweza kushindana sokoni na kuchangia maendeleo ya viwanda pamoja na kuongeza thamani ya mazao na malighafi zinazopatikana nchini.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane, VETA imeendelea kuhamasisha vijana kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili kupata ujuzi unaowawezesha kujitegemea, kuanzisha biashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia ajira na ubunifu.