Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Razack Lokina, amewahimiza Watanzania wanaotembelea Maonesho ya 33 ya Kilimo (Nane Nane 2026) kutembelea banda la UDOM ili kujifunza, kupata huduma mbalimbali na kushuhudia bunifu zinazochochea maendeleo ya sekta ya kilimo.
Prof. Lokina alitoa wito huo leo, Agosti 5, 2026, baada ya kutembelea banda la UDOM katika maonesho yanayoendelea, ambapo alipata fursa ya kujionea huduma na shughuli mbalimbali zinazotolewa na chuo.
Katika ziara hiyo, alitembelea maeneo ya udahili wa wanafunzi, huduma za afya na uchunguzi wa magonjwa, tiba lishe, pamoja na maonesho ya bunifu za kisayansi na miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha uzalishaji na maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, Prof. Lokina alisema banda la UDOM limeandaliwa kwa lengo la kuunganisha elimu, utafiti na ubunifu na mahitaji ya jamii, huku likitoa huduma zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
“Nawasihi Watanzania wote wanaotembelea Maonesho ya Nane Nane wafike katika banda la Chuo Kikuu cha Dodoma. Kuna mengi ya kujifunza, kuanzia fursa za masomo, ubunifu wa kisayansi hadi huduma za afya na uchunguzi zinazotolewa bure,” alisema Prof. Lokina.
Aidha, aliwapongeza wataalamu na watumishi wa UDOM kwa maandalizi na kazi wanayoendelea kuifanya katika maonesho hayo, akisisitiza kuwa ushiriki wa chuo unadhihirisha dhamira yake ya kutumia elimu, tafiti na ubunifu kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya taifa.
Huduma zote zinazotolewa katika banda la UDOM zitaendelea kupatikana hadi kilele cha Maonesho ya Nane Nane kitakachofanyika Agosti 8, 2026.
Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la UDOM ili kupata huduma, elimu na kujionea ubunifu unaochochea maendeleo ya Tanzania.

