Na Mwandishi Maalum, Mbinga

Kampuni ya Corteva Agriscience Tanzania Ltd, wasambazaji wa mbegu za mahindi aina ya Pannar na Pioneer, imewasisitiza wakulima wa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kuachana na matumizi ya mbegu zisizofanyiwa utafiti na badala yake kutumia mbegu bora zinazozalishwa na kampuni hiyo ili kuongeza uzalishaji na kupata mazao yenye ubora pamoja na soko la uhakika.

 

Wito huo umetolewa na Meneja wa Kanda ya Kusini wa kampuni hiyo, Sabasaba Manase, wakati akitoa elimu kwa wakulima waliotembelea banda la Corteva Agriscience katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika kijiji cha Amanimakolo, wilayani Mbinga.

 

“Ili kuongeza mavuno ni muhimu wakulima wazingatie ushauri wa wataalamu pamoja na matumizi ya mbegu bora. Wakulima wengi wa Ruvuma na maeneo ya Nyanda za Juu Kusini wanashindwa kufikia malengo ya uzalishaji kwa sababu ya kutumia mbegu zisizofanyiwa utafiti ambazo haziendani na mazingira ya kilimo katika maeneo yao,” alisema Manase.

 

Alieleza kuwa mbegu za mahindi aina ya Pannar na Pioneer zimefanyiwa utafiti wa kitaalamu, zinazingatia viwango vya ubora na usalama, na zimeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Kwa mujibu wa Manase, kampuni hiyo imeingiza sokoni aina mbalimbali za mbegu zinazofaa kwa maeneo yenye mvua chache, za wastani na nyingi ili kukidhi mahitaji ya wakulima katika mazingira tofauti ya uzalishaji.

 

Alitaja miongoni mwa mbegu hizo kuwa ni Pannar 9M-91, ambayo ina uwezo wa kutoa mahindi mawili kwa mmea, inahimili magonjwa, ina bua kubwa na inaweza kuzalisha kati ya magunia 35 hadi 40 kwa ekari moja endapo itatumika kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo.

 

Aidha, aliwataka wakulima kutembelea banda la Corteva Agriscience katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu matumizi ya mbegu bora na teknolojia mbalimbali za kuongeza tija katika kilimo.

 

Manase pia aliishauri Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima kwa kutoa ruzuku kwenye mbolea na kupunguza baadhi ya kodi za pembejeo, akisema hatua hiyo itasaidia wakulima wengi kuzalisha kwa tija bila kuingia gharama kubwa.

 

Kwa upande wake, Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Justine Nguka, amesema ushiriki wa makampuni ya mbegu katika Maonesho ya Nanenane unawapa wakulima fursa ya kupata elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora zenye tija kubwa.

 

“Tumeshuhudia ongezeko la uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo mahindi na soya kutokana na upatikanaji wa mbegu bora kutoka makampuni kama Corteva Agriscience. Wakulima sasa wanaelewa aina sahihi za mbegu zinazofaa kwa maeneo yao,” alisema Nguka.

 

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha makampuni ya mbegu kuwafikia wakulima kwa urahisi na kuhakikisha wanapata mbegu bora zitakazowaongezea uzalishaji na kuwasaidia kupata masoko ya mazao yao.

 

Naye mkulima wa kijiji cha Mpitimbi, Songea Vijijini, Betram Komba, alisema changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa mahindi ni gharama kubwa za pembejeo, hususan mbegu na mbolea, pamoja na kukosekana kwa uhakika wa soko ambapo kwa sasa kilo moja ya mahindi huuza kwa takribani shilingi 350.

 

Komba aliiomba Serikali kuongeza ruzuku kwa pembejeo za kilimo ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuwawezesha wakulima wengi kuongeza tija na kipato kupitia kilimo.