Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekabidhiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 33 kutoka Mtwara hadi Tandahimba, wenye urefu wa kilomita 92.3, ambao umelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme katika Wilaya ya Tandahimba na Jimbo la Nanyamba.

Akizungumza mkoani Mtwara Novemba 10, 2026, wakati wa ziara ya kutambulisha mkandarasi wa mradi huo ETDCO kwa viongozi wa Wilaya ya Tandahimba, Meneja wa TANESCO mkoa wa Mtwara, Mhandisi Abdul Mihambo, amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya umeme na kuboresha huduma kwa wananchi.

Mhandisi Mihambo, amesema TANESCO itaendelea kushirikiana na ETDCO ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati na kuzingatia viwango vinavyotakiwa, huku akiwashukuru viongozi wa maeneo husika kwa kuendelea kuliamini shirika hilo.

Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, amesema kuwa utekelezaji wa mradi tayari umeanza kwa kusimika nguzo za umeme, huku akieleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.

“Kutokana na kasi ya kazi tuliyoanza nayo tunatarajia kumaliza kabla ya muda uliopangwa, tunaomba ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji mradi ili kuhakikisha kazi tunamaliza kwa wakati” amesema Mhandisi Mwanja.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mtinjele, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha huduma ya umeme na kuahidi ofisi yake iko tayari kushirikiana na TANESCO, ETDCO katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mafanikio.

Kwa upande wao Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Mhe. Abdallah Chikota na Mbunge wa Tandahimba, Ahmad Katani, wameeleza dhamira yao ya kushirikiana na na ETDCO, ili kuhakikisha hakuna changamoto zitakazokwamisha utekelezaji wa mradi huo.