Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia kampuni ya ubunifu ya MaxwellTrack Technologies kimebuni mfumo wa kidijitali unaolenga kusaidia kampuni za bima na wateja wake kufuatilia mienendo ya magari na kubaini mazingira halisi ya ajali ili kurahisisha utoaji wa fidia.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mhadhiri wa UDOM na mwanzilishi wa MaxwellTrack Technologies, Jospeter Kaizilege, amesema ubunifu huo umetokana na changamoto zinazowakabili kampuni za bima kushindwa kupata taarifa sahihi kuhusu mazingira ya ajali.
Amesema mfumo huo unafuatilia mwenendo wa gari kabla na wakati wa ajali kwa kurekodi kasi ya gari, eneo lilipotokea tukio, muda wa ajali pamoja na taarifa nyingine zinazoweza kusaidia kubaini chanzo cha ajali.
“Changamoto kubwa imekuwa pale mteja anapopata ajali na kampuni ya bima kuhitaji uthibitisho wa mazingira yaliyosababisha ajali. Mfumo wetu unarekodi taarifa zote muhimu, hivyo unarahisisha kampuni ya bima kufanya maamuzi kwa kutumia ushahidi uliopo kwenye mfumo,” amesema Kaizilege.
Ameeleza kuwa tofauti na vifaa vingi vya GPS vinavyoagizwa kutoka nje ambavyo havifanyi kazi vizuri katika baadhi ya maeneo ya Afrika kutokana na changamoto za mtandao na mazingira, teknolojia hiyo imeundwa kuendana na mazingira ya Afrika na inaweza kufanya kazi hata katika maeneo yenye changamoto ya mawasiliano.
Kwa mujibu wa Kaizilege, mfumo huo utanufaisha kampuni za bima kwa kupunguza migogoro ya madai ya fidia, huku wateja wakipata uwazi zaidi kwa kuwa taarifa zote kuhusu ajali zitakuwa zimehifadhiwa na kupatikana kwa urahisi.
Amesema ubunifu huo ulianza mwaka 2022 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kama mradi wa mwisho wa masomo, kabla ya kuendelezwa kwa msaada wa programu za ubunifu za chuo hicho na kuanzishwa rasmi kupitia MaxwellTrack Technologies.
“Tumeanza rasmi kutoa huduma nchini Tanzania kwa takribani mwezi mmoja sasa na lengo letu ni kupanua huduma kwenda Kenya na Rwanda. Pia tunaendelea kushirikiana na mamlaka husika pamoja na kampuni mbalimbali za bima ili kuunganisha mfumo wetu na mifumo yao na kuhakikisha teknolojia hii inanufaisha sekta ya bima na usafirishaji kwa ujumla,” amesema Kaizilege.

