Na Hellen Mtereko,Mwanza

Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) kituo Cha Ukiriguru imewataka Maofisa Ugani kuwafundisha wakulima teknolojia zilizobuniwa na taasisi hiyo , huku ikiwahimiza wakulima kujifunza na kuzitumia ili kuongeza uzalishaji, kipato na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Hayo yamebainishwa Agosti 2,2026 na Mtafiti kutoka TARI kituo cha Ukiriguru, Mwanjia Ngangambe kwenye Banda la taasisi hiyo katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayoendelea katika uwanja wa Nyamhongoro Jijini Mwanza.

Amesema mkulima wa pamba anayezingatia teknolojia ambazo taasisi hiyo imezigundua na kuzizalisha pamoja na kanuni bora za kilimo anakuwa na uwezo wa kuvuna zaidi ya kilo 1,000 kwa ekari.

“Mafanikio kama hayo yanatokana na ubunifu wa teknolojia mpya ikiwemo nafasi bora ya upandaji ambayo imeongeza uzalisha.

Amesema taasisi hiyo inajukumu la kufanya tafiti mbalimbali na kitu chao wanamamlaka ya kufanya utafiti wa mazao mawili ya pamba na mazao ya mizizi aina ya mihogo na viazi.

“Kupitia kituo cha Ukiriguru kwa zao la pamba tumefanikiwa kugundua aina tano za mbegu bora ila kuna mbegu moja ya UKM08 ambayo ina mavuno ya kutosha kwani inavumilia magonjwa”, Amesema

Aidha, amesema kupitia kitengo cha pamba wameweza kufanya tafiti mbalimbali zonazohusiana na magonjwa pamoja na wadudu.

“Wakulima wengi wanatumia viuatilifu kwa muda mrefu na kusababisha mdudu kutengeneza usugu na ile dawa kutokufaya viziri”, Amesema Ngangambe

Kwa upande wa mazao ya mizizi wamefanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na mifumo ya mbegu kwenye mihogo pamoja na viazi vitamu ambapo ameeleza kuwa mwaka 2005 waligundua aina 27 za mbegu bora za mihogo ambazo mkulima akipanda uzalishaji unakuwa na tija kubwa.