Afisa Uzalishaji wa Mbegu wa kampuni ya Kibo Seed Co.Ltd ,Marko Msheishiwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Taso Njiro.
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .WAKULIMA kanda ya kaskazini wametakiwa kutembelea banda la kampuni ya Kibo Seed katika maonesho ya nanenane ili kuweza kupata elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora za mahindi na mbogamboga ili kuongeza uzalishaji.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Afisa Uzalishaji wa Mbegu wa kampuni ya Kibo Seed Co.Ltd ,Marko Msheishiwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Taso Njiro.
Amesema kampuni hiyo inashiriki Maonyesho ya Nanenane 2026 ikiwa na lengo la kuwaelimisha wakulima kuhusu matumizi ya mbegu bora za mahindi na mbogamboga ili kuongeza uzalishaji.
Ameongeza kuwa ,kampuni hiyo inazalisha na kusambaza mbegu za mahindi kwa kanda mbalimbali za kilimo nchini, zikiwemo kanda ya chini, ya kati na ya juu, ili kuhakikisha kila mkulima anapata mbegu zinazolingana na mazingira yake.
Akizungumzia maandalizi ya maonesho ya mwaka huu, Msheishiwa amesema yameboreshwa zaidi kuliko miaka iliyopita, ambapo mazao ya maonesho yalipandwa kwa wakati, yakatunzwa vizuri na sasa yanaonyesha matokeo halisi ambayo yatawawezesha wakulima kujifunza kwa vitendo.
Ameongeza kuwa, moja ya sifa zinazotofautisha mbegu za Kibo Seed na kampuni nyingine ni ubora wake, hususan kwa mahindi yanayofaa kuchomwa na kukobolewa, ambayo ni matamu na yanakubalika na watumiaji wengi.
Kwa upande wa uzalishaji, amesema mavuno hutegemea ukanda na aina ya mbegu inayotumika. Mbegu za ukanda wa chini zinaweza kutoa tani 2 hadi 2.5 kwa ekari, ukanda wa kati tani 3 hadi 3.5, huku ukanda wa juu ukifikia tani 4 hadi 5 endapo mkulima atafuata kanuni bora za kilimo. By
Aidha, amesema changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya wakulima ni kutokuchagua mbegu sahihi kulingana na ukanda wao wa kilimo pamoja na kutofuata kanuni za uzalishaji, ikiwemo kupanda kwa wakati, kutumia mbolea stahiki na kutunza shamba ipasavyo.
Aidha Msheishiwa ametoa wito kwa wakulima na wananchi kutembelea banda la Kibo Seed katika maonyesho ya Nanenane jijini Arusha ili kupata elimu kuhusu mbegu bora, kuona mashamba ya mfano na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa kampuni hiyo.
