Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Adil Butt wakati akizungumza katika maonesho ya nanenane katika viwanja vya Themi Njiro

 Happy Lazaro,Arusha .

Arusha .WAFUGAJI nchini wametakiwa kuzingatia ufugaji bora na wenye tija kwa kutumia mbegu bora kutoka kampuni ya West Kilimanjaro Ranching katika kuhakikisha mifugo inapata maji na malisho ya kutosha pamoja na kufuata kanuni bora za ufugaji ili kuongeza uzalishaji na kupunguza umaskini.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Adil Butt wakati akizungumza katika maonesho ya nanenane katika viwanja vya Themi Njiro .

Adil amesema kuwa, bidhaa na mbegu za mifugo zinazozalishwa na kampuni hiyo zinauzwa katika soko la ndani na nje ya nchi,ambapo wateja wao ni wafugaji binafsi, wawekezaji na taasisi mbalimbali zinazohitaji mbegu bora za mifugo kwa ajili ya kuboresha uzalishaji.

Adil ameongeza kuwa ,kwa upande wa uwajibikaji kwa jamii, kampuni hiyo imejenga ushirikiano mzuri na wananchi wanaoizunguka ranchi hiyo kupitia utoaji wa elimu, usaidizi wa miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali za kijamii. 

Aidha ameiomba Serikali kuharakisha usajili wa chanjo mbalimbali za mifugo nchini ili ziweze kupatikana kwa urahisi na kuwasaidia kudhibiti magonjwa yanayosababisha hasara kubwa katika sekta ya ufugaji.

Amesema pamoja na kuwepo kwa dawa za kutibu mifugo, upatikanaji wa chanjo bora utasaidia kuzuia magonjwa kabla hayajatokea na hivyo kupunguza matumizi ya antibiotiki pamoja na gharama za matibabu.

Aidha, wameeleza kuwa baadhi ya chanjo zinazotumika katika nchi nyingine bado hazijakamilisha taratibu za majaribio na usajili nchini Tanzania, jambo linalochelewesha matumizi yake na kuwanyima wafugaji fursa ya kunufaika na teknolojia hizo.

Mbali na changamoto ya chanjo, pia ameeleza kuwa miundombinu mibovu ya barabara, hususan katika maeneo ya Longido, inaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa usafirishaji wa mifugo kwenda kwenye masoko ambapo ukosefu wa barabara za lami unafanya usafiri kuwa mgumu na kuongeza gharama za uzalishaji.

Adil ameiomba Serikali pia kuboresha huduma za umeme katika maeneo ya wafugaji ili kuwezesha maendeleo ya shughuli za uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa za mifugo.

“Kwa ujumla tunaiomba Serikali na wadau wa sekta ya mifugo kuwekeza zaidi katika usajili wa chanjo, uboreshaji wa miundombinu ya barabara na upatikanaji wa huduma za msingi ili kuongeza tija, kulinda afya ya mifugo na kuinua kipato cha wafugaji nchini.”amesema Adil.