Na Mwandishi Wetu

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imesema inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini, ikiwemo uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa chakula wa kutosha, kuongeza ajira na kuinua kipato cha wananchi.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Dkt. Consolata Kapinga, amesema tume hiyo imejitokeza katika maonesho hayo ili kutoa elimu na taarifa kwa wananchi kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika sekta ya umwagiliaji.

Amesema miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele mwaka huu ni kuonyesha miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kueleza maendeleo ya zoezi la uchimbaji wa visima linaloendelea katika mikoa mbalimbali.

Dkt. Kapinga amesema hadi sasa Tume imefanikiwa kuchimba visima 390 katika mikoa 15 nchini, huku zoezi hilo likiendelea ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Ameeleza kuwa katika banda la Tume, wananchi wanapata fursa ya kujifunza mwongozo wa uchimbaji wa visima, taratibu za kupata huduma hiyo pamoja na kuona mifano halisi ya miundombinu mbalimbali ya umwagiliaji inayotumika katika uzalishaji wa mazao ya mbogamboga na mazao makuu ya chakula.

Kwa mujibu wa Dkt. Kapinga, Tume imeweka mipango ya kuhakikisha maeneo yote yenye uwezo wa kumwagiliwa yanatumika kwa uzalishaji ili kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza ajira na kuinua uchumi wa wakulima kupitia kilimo cha umwagiliaji.

Aidha, amesema kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kutotabirika kwa hali ya hewa, kilimo cha umwagiliaji kinaendelea kuwa suluhisho muhimu la kuhakikisha uzalishaji wa mazao unaendelea mwaka mzima na kuifanya Tanzania iendelee kuwa salama dhidi ya uhaba wa chakula. 

Dkt. Kapinga ametoa wito kwa wananchi na wadau wa sekta ya kilimo kutembelea banda la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Maonesho ya Nanenane ili kujifunza teknolojia mbalimbali za umwagiliaji na kupata taarifa zitakazowasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.