Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Peter Mwasalyanda, amewapongeza wanafunzi waliowakilisha Tanzania katika Mashindano ya Hisabati ya Afrika (PAMO) na Mashindano ya Dunia ya Hisabati (IMO) mwaka 2026 kwa kuipeperusha vyema bendera ya Taifa na kuiletea nchi heshima kubwa kimataifa.
Amesema mafanikio hayo yanaonyesha matunda ya uwekezaji wa Serikali katika elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
Mhandisi Mwasalyanda amesema TCRA imeendelea kufadhili ushiriki wa wanafunzi kupitia Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA) tangu kuanzishwa kwa mpango huo. Ameongeza kuwa mamlaka hiyo pia inaendeleza Klabu za Kidijiti shuleni na vyuoni pamoja na kutoa rasilimali za mawasiliano kwa wabunifu ili kuhamasisha maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHAHITA, Dk. Saidi Sima, alisema Tanzania imeandika historia mpya baada ya kupata matokeo bora zaidi kuwahi kuyapata katika mashindano hayo. Alieleza kuwa katika Mashindano ya Afrika yaliyofanyika Yamoussoukro, Ivory Coast, Tanzania ilijishindia medali tisa na kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi nafasi ya tano kati ya nchi 26 zilizoshiriki.
Katika Mashindano ya Dunia ya Hisabati yaliyofanyika Shanghai, China, mwanafunzi Lightness Ngiliule aliibuka msichana bora kutoka Afrika. Wanafunzi wengine waliowakilisha Tanzania ni Angel Zalwango, Sweetbert Nene, Nyandahu Leonard, Joyce Sulumo na Arqam Salim, ambao kwa pamoja waliiwakilisha vyema Tanzania miongoni mwa nchi 118 zilizoshiriki.
Aidha Mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano kati ya Serikali, TCRA na CHAHITA katika kuandaa na kufadhili wanafunzi kushiriki mashindano ya hisabati kimataifa, hatua inayozidi kuitangaza Tanzania kama taifa lenye vipaji vya kipekee katika hisabati na masomo ya STEM.
