Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) unashiriki Maonesho ya Nanenane 2026 yaliyozinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uwanja wa Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma.
Afisa Ubora wa Mafuta wa PBPA, Datson Mwantuke, amesema Wakala unatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, yakiwemo kuratibu uagizaji na upokeaji wa mafuta kwa pamoja, kusajili Kampuni za Uuzaji wa Mafuta (OMCs), kuhakiki kampuni zinazotaka kusambaza mafuta nchini na kusimamia zabuni za uagizaji wa mafuta.
Amesema wananchi pia wanaelimishwa kuhusu Mfumo wa kisasa wa SCADA, unaoiwezesha Serikali kufuatilia kwa wakati halisi kiasi cha mafuta kinachoingia nchini kupitia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Mwantuke ameeleza kuwa PBPA inatoa elimu kuhusu Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja na mchango wake katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha kwa wakati, kuongeza uwazi katika mchakato wa uagizaji na kuimarisha usalama wa nishati nchini.
PBPA inatumia maonesho hayo kuimarisha mawasiliano na wananchi pamoja na wadau, kupokea maoni na kutoa ufafanuzi kuhusu shughuli na huduma zake.
Wananchi wamekaribishwa kutembelea banda la PBPA katika Uwanja wa Nanenane, Nzuguni jijini Dodoma, ili kufahamu zaidi majukumu ya Wakala na mchango wake katika kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mafuta nchini.

