Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.), ametembelea Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma, ambapo amejionea ubunifu na maendeleo ya sekta ya kilimo pamoja na fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji.
Katika ziara hiyo, Mhe. Millya aliambatana na Mwakilishi wa Balozi wa Nigeria nchini Tanzania, Barrister Luqman Hannafi, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dkt. Vincent Mashinji, wakitembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kupata maelezo kuhusu teknolojia za kisasa za uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo.
Mhe. Millya amesema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kuunganisha wazalishaji, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo, huku yakifungua fursa za kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi kupitia ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Ziara hiyo imeonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kutumia sekta ya kilimo kama nyenzo ya kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa. Aidha, imeakisi kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu, “Tambua Soko, Ongeza Tija, kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inayohamasisha uzalishaji wenye tija, uongezaji thamani wa mazao na upanuzi wa masoko kwa maendeleo endelevu ya taifa.

