Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (MB), akimueleza Meneja wa Mikopo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Amani Shabani (kushoto), kuhusu umuhimu wa Benki hiyo kuendelea kuinua wakulima nchini, wakati alipotembelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecelaa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanayofanyika katika viwanja hivyo, Nzuguni jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, ambaye alimuongoza Mhe. Balozi Omar kutembelea Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.
Na. Farida Ramadhani na Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali ili kuongeza tija na kasi ya maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa ajili ya kuziwezesha sekta hizo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Hayo yalibainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi, Khamis Mussa Omar (MB), wakati alipotembelea Viwanja vya Dk. John Samwel Malecela vilivyopo Nzuguni, Dodoma, kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026 yanayoendelea.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana ikiwa kila sekta itafanya kazi peke yake, akisisitiza kuwa kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, biashara na sekta ya fedha zinapaswa kushirikiana ili kuongeza uzalishaji, kuchochea uchakataji wa mazao na kuimarisha huduma zinazounga mkono uzalishaji.
“Tunapaswa kuwa na mtazamo mmoja wa kukuza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao kupitia uchakataji na kuhakikisha sekta zote zinazohitajika zinashirikiana kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa. Taasisi za kifedha zinapaswa kuendelea kuunga mkono maeneo ambayo Serikali imeyapa kipaumbele ili kuongeza kasi ya uwekezaji na maendeleo ya sekta hiyo,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kufuatilia matumizi ya matrekta yaliyotolewa kwa wakulima ili kuhakikisha yanatumika katika maeneo yaliyokusudiwa na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Mhe. Balozi Omar alipongeza juhudi za wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora, lakini akasisitiza umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kuzitafutia masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza ushindani na mchango wake katika uchumi.
‘‘Pamoja na kuongeza uzalishaji, ipo haja ya kuwekeza zaidi katika utangazaji wa bidhaa, ukuzaji wa masoko na kuimarisha mazingira ya biashara ili bidhaa zinazozalishwa nchini ziweze kufahamika na kupatikana kwa urahisi katika masoko mbalimbali’’, alisisitiza Mhe. Balozi Omar.
Mhe. Balozi Omar pia alisisitiza kuwa utafiti ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta za uzalishaji, hivyo uwekezaji katika taasisi za utafiti, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), ni muhimu ili kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya mifugo kupitia teknolojia na ubunifu wenye tija.
Vilevile, alipongeza maandalizi na ubunifu uliodhihirishwa na washiriki ikionesha hatua inayopigwa katika kuendeleza sekta za uzalishaji na kwamba Maonesho hayo yamefanikiwa kufikia lengo la kuonesha fursa zilizopo pamoja na kazi inayofanywa na Serikali na wadau wake.
Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanafanyika katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecela Nzuguni, jijini Dodoma, kwa kauli mbiu isemayo ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (MB), akipokelewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, wakati alipowasili katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecelaa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanayofanyika katika viwanja hivyo Nzuguni, jijini Dodoma. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri. Maonesho hayo yana kauli mbiu ya ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (MB), na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, wakioneshwa moja ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali, wakati alipotembelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecelaa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanayofanyika katika viwanja hivyo Nzuguni, jijini Dodoma. Maonesho hayo yana kauli mbiu ya ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.

