Na John Walter -Babati
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga, ametoa siku 14 kwa Mkuu wa Wilaya ya Babati kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara kuwasilisha taarifa ya kina kuhusu malalamiko na tuhuma zinazoikabili Kiwanda cha Mbolea Minjingu, baada ya wananchi kueleza kero mbalimbali dhidi ya kampuni hiyo.
Maagizo hayo yalitolewa Julai 28, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika Kijiji cha Minjingu, wilayani Babati, ambapo wananchi walitoa malalamiko yanayohusu mazingira ya kazi, usalama wa wafanyakazi, fidia na athari za shughuli za uchimbaji wa malighafi za kutengeneza mbolea.
Sendiga amesema anahitaji kupata taarifa ya kina kuhusu malalamiko ya wananchi wanaodai nyumba zao zimeharibika kutokana na milipuko ya miamba inayofanyika wakati wa uchimbaji wa malighafi, akisisitiza kuwa taarifa hiyo iambatane na vielelezo ikiwemo picha za nyumba zilizoathirika pamoja na mahojiano ya wananchi na walalamikaji.
Pia ameagiza kufanyike uchunguzi kuhusu malalamiko ya aliyekuwa mfanyakazi wa kiwanda hicho anayelalamikia kutelekezwa baada ya kupata madhara akiwa kazini, sambamba na kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi wengine ili kubaini ukweli wa madai hayo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametaka taarifa kuhusu mikataba ya ajira ya wafanyakazi ili kujiridhisha kama Sheria za Kazi zinafuatwa, hali ya usalama mahali pa kazi, pamoja na huduma za afya na ustawi wa wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Katika maagizo yake, Sendiga pia ametaka uchunguzi ufanyike kuhusu malalamiko ya wananchi wanaodai kuwa kiwanda hicho kilichukua eneo la kijiji na kupata hati ya umiliki bila kuwashirikisha wananchi na uongozi wa kijiji husika.
Amesisitiza kuwa Serikali haitafumbia macho malalamiko yanayohusu haki za wananchi na wafanyakazi, hivyo taarifa atakayopewa baada ya siku 14 itasaidia Serikali kuchukua hatua stahiki kulingana na matokeo ya uchunguzi.
Kuhusu uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, Sendiga amesema Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ni takwa la kisheria kwa kila taasisi na kampuni inayofanya biashara nchini, hivyo Kiwanda cha Mbolea Minjingu pamoja na kampuni nyingine zote zinazofanya shughuli zake mkoani Manyara zinapaswa kutekeleza wajibu huo kwa kurejesha sehemu ya faida kwa jamii zinazozizunguka.
Aidha, amezitaka kampuni zote zilizopo mkoani Manyara kuhakikisha zinazingatia kikamilifu wajibu wa CSR ili kuchangia maendeleo ya wananchi na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya wawekezaji na jamii