Na Mwandi Maalumu RS Arusha
Vijana wanaojishughulisha na shughuli za ufugaji mkoani Arusha wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kunufaika na fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha kiuchumi na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Dkt. Sijapenda, ambaye amesema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mpango huo wa mikopo kwa lengo la kuwainua vijana wanaojihusisha na shughuli za ufugaji na kuwapa mtaji utakaowawezesha kupanua shughuli zao za uzalishaji.
Amesema kuwa katika Mkoa wa Arusha, jumla ya shilingi milioni 156 zimetolewa katika awamu ya kwanza ya mikopo hiyo kwa vijana 21 ambao tayari wamehakikiwa na kuthibitishwa kukidhi vigezo vya kunufaika na mpango huo.
Kwa upande wa utekelezaji wa mpango huo kitaifa, Dkt. Sijapenda amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 5 kati ya shilingi bilioni 23 zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya kuwawezesha vijana katika sekta ya mifugo.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha, hususan vijana, kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo hiyo katika awamu ya pili ambayo inatarajiwa kuanza Agosti 15, 2026, ili waweze kunufaika na fursa hiyo ya maendeleo.
Akifafanua masharti ya kupata mkopo huo, amesema vigezo vilivyowekwa ni rahisi ambapo mwombaji anatakiwa kuwa Mtanzania mwenye umri wa kati ya miaka 18 na 35, mwenye anuani inayotambulika pamoja na wadhamini wawili.
“Napenda kutumia nafasi hii kutoa hamasa kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi katika awamu ya pili itakayoanza Agosti 15, 2026. Vigezo ni rahisi; uwe na miaka 18 hadi 35, uwe Mtanzania, uwe na anuani na uwe na wadhamini wawili. Hakuna dhamana ya mali,” amesema Dkt. Sijapenda.
Mpango huo unatarajiwa kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za ufugaji wa kisasa, kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya mifugo, pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla

