Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ( TADB), Frank Nyabundege, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 30, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa benki hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.

Na. Meleka Kulwa, Fullshangwe Blog, Dodoma

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema kuwa kauli mbiu yake ya “Kilimo Kinabenkika” imechangia kuongeza upatikanaji wa mikopo ya kilimo nchini kutoka shilingi trilioni 1.3 hadi trilioni 5.8.Akizungumza na waandishi wa habari Julai 30, 2026, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema kuwa hapo awali wananchi wengi walikuwa wakieleza kuwa walitaka kujihusisha na kilimo lakini walishindwa kupata mikopo kutoka katika mabenki.

“Watu walikuwa wanasema jamani mimi nalima lakini ukienda kwenye mabenki huwezi kubenkika kabisa kwenye kilimo. Ndipo sisi TADB tukaja na kauli ya ‘Kilimo Kinabenkika’,” amesema Nyabundege.

Amesema kuwa kupitia kauli mbiu hiyo, sekta ya kilimo imeanza kutambulika kama shughuli yenye uwezo wa kufadhiliwa na taasisi za kifedha, jambo ambalo limeongeza kiwango cha mikopo inayotolewa kwa wakulima na wadau wengine wa kilimo nchini.

Aidha, amebainisha kuwa TADB inaendelea kushirikiana na vijana katika nyanja mbalimbali za uwezeshaji wa kiuchumi, ikiwemo utoaji wa mikopo kwa ajili ya vizimba vya samaki na boti katika maeneo ya Ziwa Victoria.

Pia ameongeza kuwa benki hiyo ni mdhamini wa mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) unaolenga kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo.

Huku akibainisha  kuwa TADB imetoa fedha kwa taasisi 19 za kifedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vijana na wanawake, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa makundi hayo muhimu katika maendeleo ya uchumi.

Aidha, amesema kuwa benki hiyo imeendelea kufungamanisha sekta ya kilimo na viwanda kupitia utoaji wa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 384.09 kwa viwanda 178 vilivyopo katika mikoa 17 ya Tanzania.

Pia, Amesema ushirikiano huo umewezesha kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kupitia uchakataji wa viwandani na hivyo kuchangia ajira, mapato ya wakulima na ukuaji wa uchumi wa taifa.

Aidha,  amesema mchango wa TADB umeendelea kuimarisha usalama wa chakula nchini kupitia uwekezaji katika uzalishaji, uhifadhi, uchakataji na masoko ya mazao. Amesema uwekezaji huo umechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula na kuiwezesha Tanzania kufikia kiwango cha kujitosheleza kwa chakula cha asilimia 130 mwaka 2025.

Amebainisha kuwa TADB imefadhili ujenzi wa maghala, vihenge, vyumba vya baridi na miundombinu ya usindikaji wa mazao, hatua iliyosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno. Huku akibainisha Kuwa  benki hiyo imewezesha ununuzi wa mazao na uunganishaji wa minyororo ya thamani, jambo lililoboresha upatikanaji wa masoko, kusaidia utulivu wa bei na kuongeza uhakika wa kipato kwa wakulima.

Pia amesema uwekezaji wa TADB katika minyororo ya thamani umechangia kuboresha lishe ya kaya kwa kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubisho, sambamba na kuimarisha usalama wa chakula na maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Ameongeza kuwa TADB inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kutekeleza dhamira yake ya kuimarisha sekta ya kilimo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Tanzania.