Lusahunga, Biharamulo – Kagera

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Mhe. Devotha Daniel, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuelekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ambayo imeendelea kuleta mabadiliko makubwa katika Mkoa wa Kagera.

Mhe. Devotha alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, aliyefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Lusahunga–Benako–Rusumo, mradi wa kimkakati unaotarajiwa kuboresha usafiri, kurahisisha biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi ndani ya Mkoa wa Kagera na maeneo jirani.

Akizungumza na wananchi wa Lusahunga wilayani Biharamulo, Mhe. Devotha alisema Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia uwekezaji mkubwa katika miradi ya miundombinu, hivyo wananchi wanapaswa kuthamini na kuunga mkono jitihada hizo.

Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano, akieleza kuwa mazingira ya utulivu ndiyo yanayowezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi na kuvutia uwekezaji zaidi.

“Tuendelee kuitunza amani ya nchi yetu, kwani maendeleo tunayoyaona leo yanatokana na utulivu uliopo. Bila amani, utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo usingewezekana kwa ufanisi,” alisema Mhe. Devotha.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, aliendelea na ukaguzi wa mradi huo ili kujiridhisha kuwa unatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na unakamilika kwa wakati, hatua ambayo inalenga kuboresha huduma za usafiri, kuimarisha biashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Kagera.