Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu ametangaza kuwa Tanzania itashiriki katika maonesho ya Wajasiliamali Wadogo ya Afrika Mashariki yatakayofayika Kigali Rwanda mwezi Oktoba mwaka huu. Amesema hayo leo 23 Julai 2026 alipozungumza na Waandishi wa Habari mjini Sumbawanga mkoa wa Rukwa.

………….

Na Neema Mtuka Sumbawanga

Rukwa: Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu – kazi ,ajira na mahusiano Deus Sangu amesema Tanzania itashiriki maonesho ya 26 ya wajasiriamali wadogowadogo,wadogo na wa kati(MSMEs)ya jumuiya ya afrika mashariki maarufu kama nguvu kazi/ jua kali yatakayofanyika Jijini Kigali – Rwanda kuanzia 30 oktoba ,2026 hadi 8 Novemba ,2026.

Akizungumza leo Julai 23 ,2026 katika ukumbi wa NSSF manispaa ya Sumbawanga Sangu amesema wajasiriamali wapatao 1,000 kutoka nchi 8 wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki watashiriki maonesho hayo.

Amesema Tanzania itawakilishwa na takribani wajasiriamali 250, na serikali itawagharamia kwa kuwasafirisha wao na bidhaa zao.

Amefafanua kuwa lengo la maonesho hayo yanayotambuliwa kama maonesho ya nguvu kazi/jua kali yanalenga kuwainua wajasiriamali wadogowadogo, wadogo na wa kati waliopo katika sekta isiyo rasmi.

“Maonesho haya yanalenga kuwawezesha wajasiriamali kurasimisha shughuli zao kwa kuwapatia fursa ya kutangaza bidhaa ,kubadilishana taarifa na uzoefu ,kukuza ujuzi ,kukuza masoko ya bidhaa na teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa na hatimaye kuongeza fursa za ajira za staha kwa watanzania.”amesema Sangu.

Ameongeza kuwa maonesho hayo yalifanyika mara ya kwanza mwezi Desemba ,1999 Jijini Arusha – Tanzania sambamba na sherehe za utiaji Saini wa mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya ya afrika mashariki uliofanyika tarehe 30,Novemba ,1999 zikiwepo nchi za Kenya ,Uganda, na Tanzania na kuhudhuriwa na wakuu wa Nchi wanachama.

Aidha Sangu ameeleza kuwa
ofisi ya waziri mkuu – kazi ,ajira na mahusiano kwa kushirikiana na wizara ya vijana ,ajira na uwezeshaji – Zanzibar, wizara , taasisi za serikali na shirikisho la vyama vya wajasiriamali Tanzania – (CISOT) imejipanga kuhakikisha inawaibia wajasiriamali mahiri watakaoiwakilisha vyema Tanzania.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally chirukile amewataka wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo kwa kujisajili kuanzia hivi sasa hadi tarehe 30 Septemba ,2026.

Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2025;na dira ya taifa ya maendeleo 2050 ya kuweka mazingira wezeshi yanayokuza ajira ujasiriamali na maendeleo ya sekta binafsi.

Baadhi ya wajasiriamali wa Sumbawanga akiwemo Charles Mwibale amesema kuwa maonesho hayo ni fursa ya kutangaza bidhaa zao ,kilimo na madini yanayopatikana mkoa wa Rukwa.

” Hii ni fursa kwetu tunakwenda kuutangaza mkoa wetu lakini pia tutabadilishana uzoefu na wajasiriamali wa mataifa mengine yanayoshiriki maonesho haya.” Amesema Mwibale