Na Hellen Mtereko,Mwanza
Kampuni ya SKYPM Solutions imewashauri wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa nchini kufanya utafiti wa kina wa madini kabla ya kuanza uchimbaji ili kupunguza hasara, kuokoa muda na kuongeza tija katika uwekezaji wao.
Akizungumza Leo Julai 23, 2026 katika maonesho ya Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania Jijini Mwanza Mkurugenzi wa SKYPM Solutions, Paul Madatta, alisema wachimbaji wengi huingia gharama kubwa kwa kuanza uchimbaji bila kuwa na taarifa sahihi za kijiolojia, hali inayowafanya kutumia fedha nyingi bila kufikia matokeo yaliyokusudiwa.
Madatta amesema kuwa uchimbaji usiozingatia matokeo ya utafiti unaweza kumfanya mchimbaji kutumia miezi mingi au hata zaidi ya mwaka kutafuta mwamba wenye uzalishaji wa dhahabu bila mafanikio.
“Utafiti wa madini ni hatua muhimu kabla ya kuanza uchimbaji unamwezesha mchimbaji kujua eneo lenye uwezekano mkubwa wa kuwa na madini na hivyo kupunguza gharama na muda wa uzalishaji,” alisema Madata.
Kwa upande wake, Mfijiolojia wa SKYPM Solutions Catherine Michibi amesema kuwa huduma za utafiti wa madini huwapa wachimbaji taarifa za kitaalamu kuhusu eneo husika, ikiwemo kina cha uchimbaji, mwelekeo wa mwamba wenye madini na mbinu salama za uchimbaji.
Michibi ameeleza kuwa taarifa hizo humwezesha mchimbaji kupanga vizuri uwekezaji wake badala ya kutumia fedha nyingi kuchimba kwa kubahatisha.
“Tunawasaidia wachimbaji kujua ni sehemu gani inafaa kuchimbwa, kina kinachoweza kufikiwa na namna bora ya kufanya uchimbaji kwa usalama, hii inapunguza gharama za uendeshaji na kuongeza nafasi ya kufikia uzalishaji kwa haraka,” alisema Michibi.
Aliongeza kuwa zamani huduma za utafiti wa madini zilikuwa zikitolewa zaidi na kampuni kutoka Afrika Kusini, Canada, Australia na Marekani, jambo lililozifanya kuwa gharama kuwa ghali na kuwafikiwa zaidi na wawekezaji wakubwa.
Hata hivyo, alisema kwa sasa kampuni za Kitanzania kama SKYPM Solutions zimeanza kutoa huduma hizo kwa gharama nafuu, hatua inayowawezesha hata wachimbaji wadogo kupata huduma za kitaalamu na kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza kwenye mitambo na shughuli za uchimbaji.
Aidha, aliwataka wachimbaji kutambua kuwa kufanya utafiti wa madini ni uwekezaji muhimu unaowasaidia kupunguza hasara, kutumia rasilimali kwa ufanisi na kuongeza tija katika shughuli za uchimbaji.
