📌Barabara mpaka milimani

📌Nauli zashuka, mabasi yaongezeka

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeufungua Mkoa wa Kigoma kwa kufanya ufikike kwa urahisi, kupunguza gharama za safari na kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wake. 

Akizungumza kwenye mikutano aliyofanya kwenye maeneo tofauti kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi inayoendelea Waziri Ulega, amesema Kigoma ya sasa ni tofauti kabisa na ile ilivyokuwa wakati Rais Samia akiingia madarakani mwaka 2021. 

Akizungumza kwa kutumia takwimu, Ulega alitoa mfano wa mtandao wa barabara za lami ambao alisema kwa miaka takribani 60 ya Uhuru, Kigoma ilikuwa na kilomita za barabara 259 za lami, lakini serikali ya Rais Samia imejenga barabara kilomita 335 kwa Mkoa huo.

“Hii maana yake ni kwamba kwa miaka mitano tu, serikali ya Rais Samia imejenga kilomita za lami ambazo ni zaidi ya kilomita zilizokuwepo kabla yake kwa miaka 60.

“Matokeo yake leo Kigoma ina mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 594 ambayo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ya kiwango kilichokuwepo zamani,” alisema Ulega. 

Ulega ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma, alifanya ukaguzi wa takribani wilaya nne tofauti za Mkoa wa Kigoma ambapo viongozi, wabunge na wananchi wa mkoa huo walieleza tofauti zilizoanza baada ya mabadiliko hayo.

Akihutubia Kasulu, Ulega alisema kwa ujumla Serikali imetumia zaidi ya shilingi Bilioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya kimkakati tisa katika Mkoa wa Kigoma peke yake.

Waziri huyo alisema kinachoendelea Kigoma ndiyo taswira pia ya maendeleo makubwa ya ujenzi yanayoendelea katika mikoa tofauti nchini Tanzania kwa sababu Rais Samia anaamini barabara ni mlango wa fursa kwa walio wengi. 

Akiwa Kigoma Vijijini, Ulega alipita katika barabara ya urefu wa km 65 ya Mkongoro – Chankere – Mwamgongo – Kagunga ya Chankere ambayo inapita kwenye njia ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki na iliyohitaji utaalamu na gharama kubwa kuijenga. Barabara hiyo imejengwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando (Baba Levo), alisema zamani nauli ya kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam ilikuwa shilingi 120,000 lakini baada ya barabara kuimarika, hivi sasa nauli imekuwa shilingi 70,000, pia muda wa safari umepungua kwa takribani saa nane, kutoka kuwa safari ya siku nzima – sawa na saa 24, na kuwa saa 16.

“Haya mambo ukiwa mtu unaishi Sinza au Kinondoni ni rahisi kudanganywa kwamba hakuna kitu kinafanyika hapa nchini. Ila watuulize sisi tuwaambie kuhusu makubwa yanayoendelea kufanyika Kigoma na kwingine,” alisema.

Naye, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Kiza Mayeye, alisema kazi ya kuufungua mkoa wa Kigoma inapaswa kuendelea kwa sababu mkoa huo ni miongoni mwa milango muhimu ya uchumi wa Tanzania. 

Mbunge huyo ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pia alizungumzia kuhusu namna usafiri ulivyorejesha utu kwa wananchi.

“Zamani ilikuwa inachukua kati ya siku nne hadi wiki moja kusafiri kutoka Kasulu hadi Manyovu ambako ni mpakani kwenda Burundi. Sasa hivi safari hiyo inachukua saa kadhaa tu. Tumerahisha maisha ya watu na biashara,” alisema mbunge huyo.

Ujenzi wa miundombinu ya barabara umetajwa pia kuwa chachu ya kuongezeka kwa shughuli nyingi za kiuchumi mkoani humo ambapo sasa viwanda zaidi vimefunguliwa na idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Gombe imeongezeka pia.