Mkurugenzi wa Kampuni ya Ovans Construction Ltd Valence Urio kushoto,akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kusaga kokoto kilichopo katika kijiji cha Lipokela wilayani Songea mkoa wa Ruvuma.

Mitambo ya kusaga kokoto katika kijiji cha Lipokela wilayani Songea kama inavyoonekana.
Na Mwandisi Maalum, Songea
BAADHI ya wananchi wanaofanya kazi katika kiwanda cha kusaga kokoto kinachomilikiwa na kampuni ya Ovans Construction Ltd katika kijiji cha Lipokela wilayani Songea,wameipongeza Serikali kuweka mazingira bora ya uwekezaji ambayo yamesaidia watu wengi hususani vijana kupata ajira,ujuzi na kuboresha maisha yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema,kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni fursa kubwa kwao na Serikali kwa ujumla kwani kimefungua milango na fursa ya kiuchumi kwa vijana Mkoani Ruvuma
George Chimimbi alisema,kiwanda hicho kimepunguza tatizo la ajira kwa vijana, na kurahisisha kazi za ujenzi wa miradi ikiwemo barabara na kumaliza changamoto kwa makampuni ya ujenzi yanayofanya kazi ndani ya mkoa wa Ruvuma kwenda mikoa mingine kununua kokoto.
Brazian Lusinde, amempongeza mwekezaji kufungua kiwanda hicho kilichosaidia wananchi hususani vijana wa wilaya ya Mbinga na Songea kupata ajira hivyo kuongeza mzunguko wa fedha kwenye vijiji vinavyopakana na kiwanda hicho.
“Tunashukuru sana kuletewa kiwanda hiki ambacho kinatuwezesha kupata kipato na kuendesha maisha yetu,mimi kabla kuwa katika kiwanda hiki nilikuwa mitaani bila kazi yoyote,maisha yangu yalikuwa magumu sana na sikuwa na shughuli yoyote ya kuzingia kipato”alisema Silinde
Naye Meneja wa kiwanda hicho Gosam Ndunguru alisema,wanazalisha aina sita za kokoto zenye ukubwa tofauti kutokana na mahitaji ya mteja kuanzia milimita 5 hadi 30.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni Ovans Construction Ltd Valence Urio alisema,kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 200 hadi 250 kwa saa moja na tangu kilipoanzishwa mwezi Mei mwaka huu kimezalisha ajira zaidi 60 za kudumu kwa vijana na wanawake wa mkoa wa Ruvuma.
Alisema, kwa sasa kiwanda hicho kimemaliza changamoto kubwa ya upatikanaji wa kokoto ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikisafirishwa kutoka mikoa mingine hapa nchini hususani Lugoba kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Urio alisema, kuanzishwa kwa kiwanda hicho kutaongeza upatikanaji wa kokoto na kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza mapato ya Serikali katika mkoa wa Ruvuma pamoja na kurahisisha kazi za ujenzi wa miradi ya barabara na majengo.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano tangu wakati wa ujenzi hadi sasa jambo lililowezesha kutimiza lengo la kuanzisha mradi huo.
“Mkoa wa Ruvuma unaendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa sekta ya ujenzi wa miundombinu,makazi na miradi ya Serikali,hivyo uwepo wa mradi huu utaongeza upatikanaji wa malighafi muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo”alisema Urio.
