Na Happy Lazaro, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amewahimiza wakulima wa zao la mbaazi kutumia teknolojia za kisasa na matokeo ya tafiti za kilimo ili kuongeza uzalishaji, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha kipato cha kaya.
 Ameyasema hayo leo  wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wakulima na wadau wa zao hilo yaliyofanyika kupitia Siku ya Mkulima wa Mbaazi iliyofanyika jijini Arusha.

Mkude amesema mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwajengea wakulima uwezo wa kutumia mbinu bora za uzalishaji, kufahamu matumizi ya mbegu bora zilizofanyiwa utafiti pamoja na kujifunza njia za kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao. 

Mkude amesema kuwa, hatua hiyo itasaidia kuongeza tija na kuimarisha uzalishaji wa zao la mbaazi katika wilaya hiyo na maeneo mengine nchini.

Ameeleza kuwa zao la mbaazi lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wakulima kutokana na mahitaji yake makubwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. 

Aidha, amesema zao hilo huchangia kuboresha rutuba ya udongo kwa uwezo wake wa kufungamanisha hewa ya nitrogen, jambo linalosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao mengine na kuimarisha usalama wa chakula.

Mkude amewataka wakulima kuendelea kushirikiana kwa karibu na watafiti pamoja na maafisa ugani ili kuhakikisha wanatumia mbegu bora na teknolojia zinazotokana na tafiti zinazoendelea kufanyika nchini.

 Amesisitiza kuwa matumizi ya maarifa na ubunifu katika kilimo ni nguzo muhimu ya kuongeza tija, kuinua kipato cha wakulima na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake Mtafiti wa mifumo ya mbegu kutoka Shirika la kitaifa la utafiti wa mahindi na ngano (CIMMYT) ,Lilian Gichuru amesema kuwa ,amewataka wakulima wa mbaazi kutumia mbegu bora, mbolea zinazofaa na kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kuinua kipato chao. 
Amesema juhudi hizo zitasaidia Tanzania kutumia kikamilifu uwezo wake mkubwa wa kuzalisha zao hilo.
Amesema TARI inaendelea kufanya tafiti za mazao mbalimbali yanayostahimili ukame, ikiwemo mahindi, ngano, karanga, mtama, mbaazi, kunde na ulezi. 
Aidha, amewataka wakulima na wadau wa biashara ya mbaazi kutopanua masoko yao kwa kutegemea eneo moja pekee, bali kuangalia fursa zilizopo ndani ya Tanzania, barani Afrika na katika masoko ya kimataifa. 
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ushindani na kuhakikisha zao hilo linawanufaisha zaidi wakulima.
Aidha ameiomba Serikali kuendelea kuimarisha huduma za ugani na kuhamasisha matumizi ya mbaazi katika programu za lishe, ikiwemo chakula shuleni, akieleza kuwa zao hilo lina virutubisho muhimu kama protini, madini ya chuma na zinki vinavyoweza kuboresha afya na lishe kwa watoto na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake  Mkurugenzi wa  kituo cha TARI SELIAN ,Dokta Caresma Chuwa amesema mafunzo hayo yanalenga kuwapa washiriki uelewa mpana kuhusu fursa zilizopo kwenye zao la mbaazi ili waweze kujikita zaidi katika uzalishaji wake.
 Chuwa amesema  kuwa hatua hiyo itachochea wakulima kupanua mashamba yao na kuongeza uzalishaji wa kibiashara kutokana na ongezeko la mahitaji ya zao hilo ndani na nje ya nchi.
Ameongeza  kuwa mbaazi ni zao lenye soko kubwa, likihitajika katika nchi jirani kama Kenya na pia katika soko la kimataifa hususan India. 
“Tanzania ina maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo cha mbaazi, yakiwemo mikoa ya Mtwara, Tanga, Manyara, Morogoro na Dodoma, jambo linaloifanya kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha kwa wingi.”amesema 
“Mbaazi si zao la biashara pekee bali pia ni chanzo muhimu cha chakula na linaweza kuongeza kipato cha wakulima ambapo  thamani ya zao hilo inaweza kuongezwa kupitia usindikaji wa bidhaa mbalimbali badala ya kutegemea matumizi ya kawaida pekee.”amesema Dokta Chuwa.
Amefafanua kuwa mbali na kutumika kupika makande, mbaazi zinaweza kusindikwa na kutengenezwa bidhaa nyingi zikiwemo keki, mikate, sambusa, pilau na vyakula vingine vinavyoongeza thamani ya zao hilo. 
Naye Mtafiti  wa zao la Mbaazi TARI -Ilonga na Mratibu wa mradi wa VACS ,Meshack  Makenge amesema kuwa ,TARI , kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kimataifa, inaendelea kutekeleza mradi wa miaka mitatu unaojulikana kama VACS  unaolenga kuboresha afya ya udongo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya jamii ya mikunde. 
“Mradi huo ulianza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2027 kwa ushirikiano wa CIMMYT na ICRISAT.”amesema .
Amesema kuwa ,kupitia mradi huo, watafiti wanaendelea kubuni na kufanya majaribio ya aina mpya za mbegu za mikunde katika vituo vya TARI Naliendele mkoani Mtwara, TARI Ilonga mkoani Morogoro na TARI Selian mkoani Arusha. 
“Lengo ni kupata mbegu zitakazokidhi mahitaji ya wakulima na kuongeza tija katika uzalishaji.”amesema .
Amesema  kuwa,mbegu mpya zinazotengenezwa zinalenga kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame unaoathiri uzalishaji wa mazao katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa mbali na kustahimili ukame, mbegu hizo pia zitakuwa na uwezo wa kupambana na magonjwa hatari yanayoathiri mikunde, hususan ugonjwa wa myauko wa Fusaria (Fusarium wilt), pamoja na baadhi ya wadudu waharibifu ambao wamekuwa wakisababisha hasara kubwa kwa wakulima.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima  walieleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuongeza thamani ya mazao yao, kupanua soko la ndani na kuhamasisha matumizi ya vyakula vya mikunde katika familia na shule. 
Walisema hatua hiyo itasaidia kuboresha lishe, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza kipato cha kaya pamoja na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.