NA DENIS MLOWE, IRINGA
WANANCHI wa vijiji vya Mwambao, Welu, Lupalama na Kibebe katika Kata ya Ulanda, Jimbo la Kalenga, wamemweleza Mbunge wao, Jackson Kiswaga, changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, ubovu wa barabara, ukosefu wa umeme katika baadhi ya vitongoji, gharama kubwa za mbolea, kushuka kwa bei za mazao pamoja na gharama za urasimishaji wa ardhi.
Wakizungumza katika mikutano ya hadhara aliyofanyika katika vijiji hivyo wakati wa ziara ya mbunge huyo, wananchi walimpongeza kwa juhudi za maendeleo zilizofanyika katika sekta mbalimbali, lakini wakasisitiza kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele.
Jackson Nziku alisema wananchi wanathamini ujenzi wa zahanati na matengenezo ya barabara yaliyofanyika katika eneo lao, lakini bado kipande cha barabara kinachoelekea shuleni ya Welu na kwenye kivuko cha Mwambao hakijakamilika na hivyo kuendelea kuwasumbua hasa kipindi cha mvua.
“Tunaomba kipande kilichobaki kikamilishwe ili wananchi na wanafunzi waweze kupita kwa urahisi. Muombaji hachoki,” alisema.
Kwa upande wake, Mchungaji Isaac Kapoma alisema pamoja na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo, bado barabara inayounganisha Kata ya Ulanda na maeneo jirani haijaimarishwa kwa kujengwa makaravati, jambo linalosababisha magari kushindwa kupita wakati wa mvua.
Aidha, wananchi walieleza kuwa gharama za mbolea zimeendelea kupanda na kuwa mzigo mkubwa kwa wakulima, huku wakiiomba Serikali kurejesha au kuongeza ruzuku ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Mbali na hilo, walilalamikia kushuka kwa bei za mazao ya kilimo, wakisema hali hiyo imeathiri kipato cha wakulima ambao hutegemea mazao kwa ajili ya kuendesha familia na kusomesha watoto.
Katika sekta ya nishati, wananchi walidai kuwa walitekeleza maelekezo ya TANESCO kwa kufanya wiring majumbani baada ya kuahidiwa kuunganishiwa umeme, lakini baadhi ya vitongoji bado havijafikiwa na huduma hiyo licha ya nguzo kufikishwa katika maeneo machache.
Pia walieleza wasiwasi wao kuhusu gharama za urasimishaji wa ardhi, wakisema kiasi kinachotozwa ni kikubwa kwa wananchi wa vijijini na kuomba Serikali kutafuta utaratibu utakaowezesha wengi zaidi kupata hati za maeneo yao.
Akijibu hoja hizo, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, alisema changamoto ya maji katika vijiji hivyo inafahamika na tayari Serikali imeingiza mradi wa maji wa Kalenga–Tanangozi (TOSA) katika mipango ya utekelezaji ili kuongeza uwezo wa kuwahudumia wananchi wa maeneo husika.
Alisema pamoja na changamoto ya upatikanaji wa fedha za utekelezaji, yeye kwa kushirikiana na viongozi wa jimbo wataendelea kufuatilia kwa karibu ili mradi huo utekelezwe haraka na kuondoa tatizo la muda mrefu la maji.
Kuhusu barabara, Kiswaga alisema Jimbo la Kalenga hupokea takribani shilingi bilioni 3.5 kwa mwaka kwa ajili ya matengenezo ya zaidi ya kilometa 900 za barabara, fedha ambazo hazitoshelezi kutekeleza mahitaji yote yaliyopo.
Alifafanua kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali hulazimika kuweka kipaumbele kwenye maeneo yaliyoharibika zaidi na yasiyopitika kabisa, huku akibainisha kuwa Serikali imeombwa kufanya tathmini upya ya mtandao wa barabara ili kuongeza fedha za matengenezo.
Kiswaga alisema mkakati wa muda mrefu ni kubadilisha barabara nyingi za udongo kuwa za changarawe ili zipunguze gharama za matengenezo na zidumu kwa muda mrefu.
Akizungumzia mbolea, alisema Serikali bado inaendelea kutoa ruzuku kwa baadhi ya aina muhimu za mbolea kama Urea na DAP, lakini aina nyingine ziliondolewa baada ya kipindi cha mpito cha kuwajengea uwezo wakulima kutumia mbolea mpya.
Alisema wabunge wameendelea kuishauri Serikali kutafuta fedha zaidi ili kuongeza ruzuku kutokana na changamoto kubwa zinazowakabili wakulima, hususan katika maeneo yanayotegemea kilimo kama Kalenga.
Kuhusu umeme, Kiswaga alisema atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya REA na TANESCO ili kuhakikisha vitongoji ambavyo havijafikiwa vinapatiwa huduma hiyo kama ilivyopangwa.
Aidha, kuhusu urasimishaji wa ardhi, alisema Serikali inaendelea kuingiza vijiji vingi katika mpango wa kupima na kusajili ardhi, huku akisisitiza kuwa changamoto kubwa imekuwa ni gharama za utekelezaji na upatikanaji wa fedha.
Akigusia sekta ya afya, Kiswaga alisema Serikali imeendelea kuboresha mfumo wa bima ya afya kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa gharama nafuu, baada ya kupokea maoni kutoka kwa wabunge na wananchi waliopinga gharama zilizokuwa zimependekezwa awali.
Aliahidi kuendelea kushirikiana na wananchi na viongozi wa maeneo husika kuhakikisha changamoto zilizowasilishwa zinafanyiwa kazi hatua kwa hatua kadri Serikali inavyopata uwezo wa kifedha.
Katika mikutano hiyo Kiswaga alitoa mabati 70 kwa kijiji cha Mwambao ili kuweza kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Kijiji na kuyakabidhi wa viongozi wa kijiji hicho.