Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Balozi Anda Filip, amewasili Tanzania usiku wa kuamkia leo Septemba 30, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya Mkutano wa 153 wa IPU utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 9, 2026.

Balozi Filip alipokelewa na Balozi wa Tanzania anayeshughulikia Dawati la IPU Geneva, Mhe. Hoyce Temu, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya Maandalizi Ndg. Daniel Eliufoo.

Balozi Filip, raia wa Romania, alichaguliwa Aprili 2026 Mjini Istanbul na kuingia madarakani Julai 1, 2026, anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Sekretarieti ya IPU katika historia ya miaka 137 ya taasisi hiyo.

Mkutano wa 153 utajadili kaulimbiu isemayo “Enhancing good governance and empowering communities through inclusivity, trust and opportunities for all” na utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 2,000 kutoka Mabunge 183 wanachama wa IPU ambao ni Maspika, Wabunge, Makatibu na Maafisa mbalimbali.