Happy Lazaro, Arusha.

Arusha .Serikali imeweka bayana kuwa mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yatategemea kwa kiwango kikubwa mchango wa Mawakili wa Serikali, hususan katika kusimamia masuala ya kisheria yanayohusu miradi mikubwa ya maendeleo na uwekezaji.

Akifunga mafunzo maalumu ya siku tatu kwa Mawakili wa Serikali yaliyofanyika jijini Arusha, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, amesema wakati umefika kwa mawakili hao kuwa zaidi ya washauri wa sheria na kuwa wadau muhimu wa maendeleo ya Taifa kupitia utaalamu wao.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamekusudiwa kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya zinazojitokeza katika mazingira ya utawala na uchumi, huku akiwataka kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha usimamizi wa mikataba, utoaji wa ushauri wa kisheria na utatuzi wa migogoro kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi.

Kwa mujibu wa Mhe. Katimba, Serikali inahitaji wataalamu wa sheria wanaoweza kufanya uchambuzi wa kina, kufikiri kimkakati na kuhakikisha kila mkataba au uamuzi wa kisheria unalinda rasilimali za Taifa na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Amesema anaamini washiriki wa mafunzo hayo watakuwa chachu ya mabadiliko katika taasisi wanazotoka na wataongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao, hatua itakayosaidia kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. 

Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel M. Maneno, amesema programu hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa ya taaluma ya sheria, ikijumuisha mada kuhusu mikataba ya kimkakati, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), usimamizi wa vihatarishi vya kisheria, usuluhishi wa migogoro pamoja na matumizi ya Akili Unde (AI) katika utoaji wa huduma za kisheria.

Aidha, amewataka Mawakili wa Serikali kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kuongeza ubora wa utendaji wa taaluma ya sheria, ikiwa ni pamoja na kusoma na kuyatumia mafunzo yaliyomo katika kitabu Mama Samia Doctrine of Law ili kuimarisha uchambuzi wa masuala ya kisheria na usimamizi wa mikataba ya Serikali.

Mafunzo hayo ya Bespoke 2026, yaliyobeba kaulimbiu “Repositioning State Attorneys for Strategic Legal Leadership in Realizing Tanzania Development Vision 2050,” yaliwakutanisha Mawakili wa Serikali kutoka wizara, taasisi, wakala na mamlaka za serikali za mitaa kwa lengo la kuongeza ufanisi wa uongozi wa kisheria katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya Taifa.