Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya ameitaka Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma na kujitangaza ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu yake na kurahisisha upatikanaji wa huduma, ikiwemo vibali vya ujenzi.

Eng. Kasekenya ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma, katika ziara yake ya kukagua utendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi.

Amesema AQRB ni Taasisi muhimu katika sekta ya ujenzi, hivyo inapaswa kuunganisha mifumo yake na Taasisi nyingine za Serikali zinazofanya kazi za ujenzi ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi.

“AQRB jitangazeni zaidi kupitia majukwaa ya kidigitali, mitandao ya kijamii na semina kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara na viongozi wa kisiasa, ili wananchi waielewe vizuri nafasi yenu na kunufaika na huduma zinazotolewa,” amesema Mhandisi Kasekenya 

Aidha,ameishauri Bodi hiyo kushirikiana na Serikali katika kuandaa Sheria ya Vibali vya Ujenzi (Building Act), ambayo itasaidia kuboresha mfumo wa utoaji vibali na kuimarisha utendaji wa sekta ya ujenzi.

Naibu Waziri huyo amesisitiza AQRB kutekeleza program za mafunzo kwa watumishi wake na kuwataka kufanyakazi kwa biidii, ubunifu na maadili ili kuleta tija.

Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa AQRB, Arch.Dkt.Daniel Matondo amesema Bodi hiyo imeendelea kusajili wataalamu, makampuni na miradi mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo endelevu ya kitaaluma yaliyofanyika katika mikoa ya Arusha na Morogoro.

Amesema pia AQRB imeimarisha ushirikiano na jumuiya za kitaaluma za kimataifa, ikiwemo SADC, hatua inayochangia kuongeza ushindani na kubadilishana uzoefu katika sekta ya ujenzi.