Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetoa msamaha wa tozo kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango na tozo zinazotokana na ucheleweshaji wa kuwasilisha michango ili kutoa unafuu kwa waajiri na kuwasaidia kuelekeza rasilimali fedha kwenye uzalishaji, uwekezaji, kuongeza tija na kukuza biashara.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba ametangaza msamaha huo wakati akizungumza na Waandishi wa Habarı Julai 17, 2026 jijini Dar es Salaam ambapo ameeleza kuwa Mfuko huo umeidhinisha msamaha wa tozo kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango kwa kipindi cha miezi saba kuanzia tarehe 1 Juni 2026 hadi tarehe 31 Desemba 2026 kwa kuzingatia masharti ambayo yamegawanywa katika makundi manne.

“Ni muhimu kusisitiza kuwa fursa hii haitolewi mara kwa mara, kwa kawaida hutolewa baada ya kupita kipindi fulani ambapo mara ya mwisho ilitolewa mwaka 2024. Hivyo, ninawasihi waajiri wasisubiri hadi muda wa mwisho, bali watumie fursa hii mapema ili wanufaike na viwango vya juu vya msamaha vinavyotolewa. Aidha, natoa wito kwa waajiri wote kuendelea kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ili kuwaepusha na gharama za tozo na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao kwa wakati”, amesema Mkurugenzi Bw. Mshomba.

Amefafanua masharti ya msamaha huo ikiwemo: waajiri watakaolipa malimbikizo yote ya michango ya wanachama (malimbikizo ya msingi) wanayodaiwa kabla au ifikapo tarehe 31 Agosti, 2026 na kuendelea kulipa michango kwa wakati mpaka ifikapo tarehe 31 Desemba, 2026, watasamehewa tozo wanazodaiwa kwa asilimia 100 huku waajiri watakaolipa malimbikizo yote ya michango ya wanachama (malimbikizo ya msingi) wanayodaiwa kabla au ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2026 na kuendelea kulipa michango kwa wakati mpaka ifikapo tarehe 31 Desemba, 2026 watasamehewa tozo wanazodaiwa kwa asilimia 75.

Masharti mengine ni waajiri watakaolipa malimbikizo yote ya michango ya wanachama (malimbikizo ya msingi) wanayodaiwa kabla au ifikapo tarehe 31 Desemba, 2026, watasamehewa tozo wanazodaiwa kwa asilimia 50 na waajiri wote ambao hawana malimbikizo yoyote ya michango ya wanachama (malimbikizo ya msingi) wanayodaiwa mpaka kufikia tarehe 31 Mei, 2026 na kuendelea kulipa michango kwa wakati mpaka ifikapo tarehe 31 Desemba, 2026 watasamehewa tozo wanazodaiwa kwa asilimia 100.

Mkurugenzi Mshomba ametumia fursa hiyo kuwahimiza waajiri wote wenye malimbikizo ya michango kutumia kikamilifu fursa hiyo kwani ni nafasi ya kupunguza gharama zinazotokana na tozo, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na kuboresha ustawi wa wafanyakazi wao.

Katika upande mwingine, Bw. Mshomba amewahimiza wafanyakazi wote kufuatilia michango yao kila mwezi kupitia mifumo ya kidijitali ya Mfuko ambayo ni NSSF App, NSSF Portal na WhatsApp Chatbot (+255 756 140 140) kwa kuandika neno “Habari” au “Hello” na kufuata maelekezo.