Serikali imeendelea kukamilisha maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM and Infra for Africa Forum), utakaofanyika Agosti 5 na 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, alipokutana na Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo kwa lengo la kutathmini maendeleo ya maandalizi na kuhakikisha shughuli zote zinakamilika kwa wakati.
Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, jijini Dar es Salaam.
Kamishna Bade aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara hiyo, Bi. Rose Kitandula, ambaye alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa kikao.
Katika kikao hicho, wajumbe wa kamati waliwasilisha taarifa ya hatua mbalimbali zilizofikiwa katika maandalizi ya mkutano, ikiwemo utekelezaji wa majukumu ya kiufundi, uratibu wa washiriki na mipango ya kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji, na hivyo kuleta mafanikio ya mkutano huo wa kimataifa.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, viongozi hao walieleza kuridhishwa na kasi ya maandalizi, huku wakisisitiza umuhimu wa kukamilisha kwa wakati majukumu yaliyosalia ili kuhakikisha mkutano unafanyika kwa ufanisi na kuacha manufaa makubwa kwa Taifa.
Mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 1,200, wakiwemo viongozi wa Serikali, wanahisa wa Africa50, wawakilishi wa taasisi za fedha, wawekezaji wa kimataifa na wadau wa sekta binafsi kutoka ndani na nje ya Afrika.
Mbali na kujadili fursa za maendeleo ya miundombinu barani Afrika, mkutano huo pia utakuwa jukwaa muhimu kwa Tanzania kutangaza fursa za uwekezaji, vivutio vya utalii na miradi ya kimkakati inayolenga kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi.
Serikali inaamini kuwa, kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutaimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki, huku ukichochea ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

