Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Jonathan Nkwabi akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Crispin Kahesa tuzo ya mshindi wa pili katika kundi la watoa huduma za afya na matibabu kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayomalizika leo katika viwanja vya Julius Nyerere vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Crispin Kahesa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyazi wa taasisi hiyo mara baada ya kukabidhiwa tuzo ya mshindi wa pili katika kundi la watoa huduma za afya na matibabu kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayomalizika leo katika viwanja vya Julius Nyerere vilivyopo jijini Dar es Salaam.

 Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

14/7/2026 Zaidi ya watu 4000 wamepata huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayomalizika leo katika viwanja vya Julius Nyerere vilivyopo jijini Dar es Salaam.

 Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Crispin Kahesa wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu huduma wanazozitoa katika maonesho hayo.

 Dkt. Kahesa alisema kati ya wagonjwa waliowaona 670 walikutwa na viashiria vya awali vya magonjwa ya saratani na kupewa rufaa ya kwenda katika taasisi hiyo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na vipimo vya zaidi

 “Kati ya watu 670 tuliowapa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi ya Saratani Oceanroad (ORCI) wanawake walikuwa 400 na wanaume 270 wengi wao walikuwa na viashiria vya awali vya saratani ya mlango wa kizazi na tezi dume. Ninawaomba wananchi wajenge tabia ya kupima saratani mara kwa mara kwani saratani ikigundulika mapema inatibika”.

 “Katika maonesho haya tunatoa huduma bila malipo za uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti, mlango wa kizazi, tezi dume, elimu ya lishe na saratani, ushauri wa kitaalamu wa magonjwa ya sarani pamoja na matumizi sahihi ya dawa”, alisema Dkt. Kahesa.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Biashara wa Mamlaka ya Biashara (TANTRADE) Jonathan Nkwabi aliishukuru ORCI kwa huduma waliyoitoa katika maonesho hayo kwani imewasadia wananchi wengi kufahamu hali za afya zao.

 “ORCI wamepata tuzo ya mshindi wa pili katika kundi la watoa huduma za afya na matibabu, hii ni kutokana na huduma bora waliyoitoa ya uchunguzi wa magonjwa ya saratani kwa wananchi, tunatambua mchango wao”, alisema Nkwabi.

Nkwabi alitoa wito kwa wananchi kutembelea maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka ili waweze kupata huduma mbalimbali zikiwemo za kupima afya zao. 

Kwa upande wao wananchi waliopata huduma katika banda hilo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali za afya zao na kupata elimu ya magonjwa ya saratani.

“Katika maisha yangu sijawahi kupima saratani, nashukuru nimefika katika banda hili la ORCI nimefanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti. Ninawaomba kina mama wenzangu wakisikia kuna upimaji wa aina hii wasiogope waende kupima afya zao”, alisema Esta Sanga mkazi wa Temeke. 

“Ninawashukuru sana wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa huduma nzuri waliyonipa, nimefika hapa nimepima tezi dume kwa njia ya damu nimekutwa sina tatizo lolote lile”, alishukuru Mohamed Mbwana mkazi wa Chalinze. 

Katika maonesho hayo Taasisi ya Satani Ocean Road (ORCI) iliibuka mshindi wa pili katika kundi la watoa huduma za afya na matibabu.