Na John Walter -BABATI
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kuhusu maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), hususan kwa vijana wa rika balehe, akieleza kuwa ugonjwa huo bado upo na unahitaji tahadhari pamoja na mabadiliko ya tabia.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa afua za UKIMWI katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara iliyopo mtaa wa Miomboni, Halmashauri ya Mji wa Babati, Mwang’onda amesema ni muhimu kuendelea kuandaa makongamano na kampeni za kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima VVU, kupata ushauri nasaha na kufahamu hali zao za afya.
Amesema watumishi wa afya na wadau wanaotekeleza afua za UKIMWI wanafanya kazi ya kitume waliyopewa na Mwenyezi Mungu ya kuokoa maisha ya watu, hivyo wanapaswa kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu na kujituma katika kuwasaidia wengine.
“UKIMWI bado upo. Vijana, hasa wa rika balehe, wanapaswa kuwa makini na kuendelea kupewa elimu sahihi ili kujikinga na maambukizi mapya. Wale wanaotoa huduma hii wanafanya kazi ya kitume, waendelee kuwahudumia wananchi kwa moyo na kujituma,” alisema Mwang’onda.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za UKIMWI, Dkt. Emmanuel Mkonyi kutoka Kitengo cha UKIMWI cha Halmashauri ya Mji wa Babati amesema kiwango cha maambukizi ya VVU kwa Tanzania Bara ni asilimia 4.8, huku Halmashauri ya Mji wa Babati ikiwa na kiwango cha asilimia 1.2.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha utekelezaji wa programu hiyo, jumla ya wateja 17,860 walipimwa VVU, wakiwemo wanaume 7,966 na wanawake 9,894. Kati yao, watu 242 walibainika kuwa na maambukizi ya VVU, wakiwemo wanaume 79 na wanawake 163, na wote walianzishiwa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV).
Dkt. Mkonyi amesema Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU pamoja na kuhamasisha wananchi kupima kwa hiari. Aidha, kwa mwaka 2026 jumla ya kondomu 666,400 zimesambazwa kwa wananchi kama sehemu ya juhudi za kuzuia maambukizi mapya ya VVU.
