NA DENIS MLOWE, IRINGA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, amesema Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa imeanza ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama katika Wilaya ya Kilolo ikiwa ni sehemu ya wajibu wa chama kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inafikia malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumza baada ya Kamati ya Siasa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo Shule Mpya ya Sekondari Ng’uruhe na ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kilolo, Daudi alisema wajumbe wa kamati wameridhishwa na ubora wa miradi hiyo na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuitunza ili idumu kwa muda mrefu.
Alisema Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya, mabweni, maabara na vyuo vya ufundi, hatua ambayo inalenga kuongeza fursa za elimu na kuwaandaa vijana kuwa wataalamu wa baadaye
.
“Tuko katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Chama ndicho kinachosimamia Serikali na utekelezaji wa ilani yake, hivyo ni wajibu wetu kujiridhisha kuwa miradi inayotekelezwa inawanufaisha wananchi.
Tumeridhishwa na shule hii mpya ya Ng’uruhe na tunaamini wananchi wataitunza ili iendelee kutoa huduma kwa vizazi vingi,” alisema Daudi.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo ya taifa kwani kupitia shule hizo watoto watapata fursa ya kuwa viongozi, madaktari, wahandisi, walimu na wataalamu mbalimbali watakaolijenga taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu katika halmashauri zote za mkoa kwa kujenga shule mpya, mabweni, maabara na miundombinu mingine muhimu.
Alisema Shule ya Sekondari Ng’uruhe imejengwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Makwema pamoja na kupunguza umbali ambao wanafunzi walikuwa wakitembea kufuata elimu.
“Hapa Serikali imeleta zaidi ya shilingi milioni 200 kuhakikisha shule hii inajengwa na kuwahudumia watoto wa maeneo haya lengo ni kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi na kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza,” alisema Kheri James.
Katika taarifa ya mradi iliyosomwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Makwema, Newas Mtenga, ilielezwa kuwa Shule ya Sekondari Ng’uruhe yenye usajili namba S.8667 ina walimu watano na wanafunzi 68 waliohamishwa kutoka Shule ya Sekondari Makwema.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’uruhe, Martin Kifiyasi, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ujenzi wa shule hiyo, akisema imeondoa changamoto ya wanafunzi wengi waliokuwa wakisoma katika Shule ya Sekondari Makwema iliyokuwa na zaidi ya wanafunzi 600..
Naye mwananchi wa Kijiji cha Ng’uruhe, Merina Kisoma, alisema shule hiyo imewapunguzia wazazi gharama za usafiri na kupunguza utoro wa wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata elimu.
Mbali na shule hiyo, Kamati ya Siasa pia ilikagua maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kilolo kinachojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyowasilishwa na Afisa Udhibiti Ubora wa Shule Wilaya ya Kilolo, Alto S. Kinunda, hadi Julai 9, mwaka huu serikali ilikuwa imepokea zaidi ya shilingi milioni 777 kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo zaidi ya shilingi milioni 608 zimetumika na ujenzi umefikia asilimia 76.
Ziara hiyo itaendelea katika wilaya zote za mkoa wa Iringa kuweza kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.

