Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia (Mama Samia Doctrine of Law); kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Hamza Johari kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) Jijini Arusha tarehe 13 Julai, 2026. Kitabu hicho kinaelezea historia, falsafa na mafanikio ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.

………

Na Paschal Dotto- MAELEZO.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka Mawakili kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo, akisisitiza kuwa
wana wajibu wa kulinda maslahi ya taifa.

Rais Samia ametoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa Mawakili unaofanyika jijini Arusha, leo Julai 13, 2026.

Mkutano huo uliowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya sheria umelenga kujadili maendeleo ya taaluma hiyo pamoja na mchango wake katika kuimarisha utawala wa sheria nchini.

Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa mawakili kutumia taaluma yao kuimarisha haki, amani na maendeleo ya Taifa badala ya kuruhusu tofauti za kimtazamo kuathiri utekelezaji wa wajibu wao wa kitaaluma akisema kuwa Tanzania ni moja, ikiharibika hakuna Tanzania nyingine.

“Niwaombe sana ndugu zangu, sisi ni Watanzania, Tanzania ni yetu sisi, si ya mtu mwingine, ikiendelea ikiwa vizuri ni yetu, tukiivuruga ikaharibika ni yetu pia kwa hiyo niwaombe fanyeni kazi mkijua nyinyi ni watanzania hapa ndipo kwetu hakuna Tanzania nyingine”, Rais. Dkt. Samia.

Alieleza kuwa, Tanzania inaendelea kujenga misingi imara ya utawala wa sheria, hivyo mchango wa mawakili unahitajika katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa usawa, huku maslahi ya Taifa yakiendelea kulindwa hususani utekelezaji wa Dira 2050 wakiwa ni wadau muhimu katika safari hiyo iliyoanza Julai 1, 2026.

Aidha, Rais aliwahimiza mawakili kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za haki katika kuimarisha mfumo wa sheria, kuongeza imani ya wananchi kwa vyombo vya utoaji haki na kujenga mazingira yanayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mkutano huo umewakutanisha mawakili kutoka sehemu mbalimbali za nchi pamoja na viongozi wa Serikali na wadau wa sekta ya sheria, ukijadili fursa na changamoto zinazoikabili taaluma ya sheria pamoja na hatua za kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za kisheria nchini.

Mwisho