Mwenge wa Uhuru wakagua miradi 48 ya  Bilioni 27.4
Mkoa wasajili vikundi 1,400 kwenye mfumo wa NeST sawa na 133% kwa zidio la vikundi 350
………….
Na Elinipa Lupembe  Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.CPA Amos Gabriel Makalla ameukabidhi Mwenge wa Uhuru 2026 kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Omari Dendegu, mara baada ya kuhitimisha mbio zake katika mkoa wa Arusha, kwenye uwanja wa Soko la Getini Mirerani, asubuhi ya leo Julai 12,2026
Amesema kuwa, Mwenge wa Uhuru 2026 ukiwa Mkoani Arusha umekimbizwa umbali wa Km 1,118.15 na kukagua jumla ya miradi 48 katika sekta za afya, maji, barabara, uwezeshaji wananchi kiuchumi na uwekezaji wa sekta binafsi  yenye thamani ya shilingi Bilioni 27.4, pamoja na kutoa Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2026 na jumbe za kudumu za Mwenge Uhuru.
CPA Makalla amebainisha kuwa, Mwenge wa Uhuru katika kuhakikisha makundi maalumu yananufaika na zabuni za Taasisi za Umma, Mkoa wa Arusha umevuka lengo la usajili kwa kusajili jumla ya vikundi 1,400 kwenye mfumo wa manunuzi ya Serikali – NeST, sawa na asilimia 133 kwa zidio la vikundi 350 kutoka lengo la kusajili vikundi 1,050
Aidha, Mhe. Makalla amewapongeza vijana 6 wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa wakiongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda kwa kazi kubwa ma nzuri waliyoifanya wakiwa Arusha na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa, kwa maendeleo ya wanaArusha na Taifa kwa ujumla wake
Hata hivyo, CPA Makalla amewasisitiza wananchi wa mkoa huo, kuendelea kuenzi Falsafa ya Mwenge wa Uhuru kwa kutunza tunu za Taifa, kulinda amani, umoja na kudumisha mshikamano kwa maendeleo ya mkoa na Taifa nzima la Tanzania