Na. Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

SERIKALI imewataka Watanzania kuendelea kulinda na kudumisha amani ya nchi kwa kutambua kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, huku ikisisitiza kuwa jukumu hilo linamhusu kila mwananchi bila kujali dini, kabila au itikadi za kisiasa.

Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, profesa Palamagamba Kabudi, wakati wa Ibada ya Siku Maalumu ya Wanaume (AMO Big Day) iliyofanyika katika Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA), Mwenge, tarehe 11 Julai, 2026 jijini Dar es Salaam.

Dkt. Nchemba alisema ulinzi wa amani unapaswa kupewa kipaumbele na kuwa ajenda namba moja ya kitaifa kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, unaowezesha wananchi kuishi kwa utulivu, kufanya kazi kwa bidii na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Alisema kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani kwa kuheshimu sheria za nchi, kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na utulivu wa nchi.

“Suala la ulinzi wa amani lipewe kipaumbele na kwa kila mmoja liwe ajenda namba moja ya kitaifa. Watanzania wote tutambue kuwa tunao wajibu wa kulinda amani yetu,” alisema.

Aidha, Dkt. Nchemba aliwataka viongozi wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha wananchi kudumisha amani, upendo, mshikamano na maadili mema kupitia mafundisho yao.

Alisema viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye umoja na mshikamano, hivyo wanapaswa kuendelea kuhubiri ujumbe wa amani na kuhimiza wananchi kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa taifa.

“Viongozi wa dini endeleeni kuhubiri kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na upendo miongoni mwa wanajamii. Ninawasihi sana katika hili, shirikianeni na Serikali kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu. Suala la ulinzi wa amani halina mbadala; sote kwa pamoja tuendelee kuweka msisitizo katika kulinda amani ya nchi,” alisema.

Alisema Tanzania imeendelea kujijengea heshima ndani na nje ya nchi kutokana na historia yake ya amani, umoja na mshikamano, hali iliyowezesha kuvutia uwekezaji, kukuza biashara, kuboresha utoaji wa huduma za jamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchemba aliwapongeza waumini wa Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA) Mwenge kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la kisasa la ibada, akisema ni ushahidi wa imani yao, mshikamano na kujitoa katika kazi ya Mungu.

“Hili ni jambo la kujivunia. Ni alama ya imani yenu thabiti, mshikamano wenu wa kijamii na bidii yenu ya kujitoa kwa kazi ya Mungu,” alisema.