Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Julai 11,2026
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, CPA Subira Mgalu, ameeleza ipo haja ya kuwaandaa vijana mapema ili waweze kunufaika na fursa za ajira na uwekezaji zitakazotokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuibadilisha Bagamoyo kuwa kitovu cha uchumi.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha wakuu wa shule zote za sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo kilicholenga kutathmini matokeo ya Kidato cha Sita ya mwaka 2026.
Alibainisha Serikali tayari imeanza kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanza rasmi Julai 1, 2026, ukiwa sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hatua ambayo itaenda sambamba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika na miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa Bandari Mpya ya Bagamoyo, Mji wa Viwanda katika eneo la Serikali la Zinga, reli ya kisasa, barabara pamoja na miundombinu mingine itakayovutia wawekezaji na kuongeza nafasi za ajira.
“Nimeiangalia Bagamoyo ya kesho, Miradi hii sasa ni ya uhakika na utekelezaji wake umeanza” kasi ya kuwaleta wawekezaji inaongezeka, na miradi hii itahitaji makampuni mbalimbali pamoja na nguvu kazi ya vijana wetu”.
“Nimeona ni wajibu wangu kama mwakilishi wa wananchi kusaidia kuwaandaa vijana wetu ili wasiwe watazamaji wala wasindikizaji wa maendeleo,” alifafanua Mgalu.
Alieleza kuwa dhamira hiyo inaendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania, hususan vijana.
Mgalu alisisitiza kuwa maandalizi ya vijana yanapaswa kuanza sasa kupitia elimu, mafunzo ya ujuzi na kuwawezesha kushindana katika soko la ajira litakalotokana na utekelezaji wa miradi hiyo.
“Nitasikitika kuona nafasi za ajira zipo, lakini sisi hatuna vijana wa kuwashindanisha kwa sababu hatukuwaandaa mapema, hilo ndilo tunalolipa kipaumbele leo, ili mwisho wa siku tuone wana Bagamoyo wanakuwa sehemu ya mafanikio ya miradi hii mikubwa,” alieleza Mgalu.

