Na Happy Lazaro, Arusha 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inafikia lengo la kukusanya Sh trilioni 41.4 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika mwaka wa fedha wa Julai 2026 hadi Juni 2027.

Akizungumza katika kikao cha viongozi wa TRA, Kamishna Mkuu amesema taasisi hiyo imepitia utekelezaji wa mipango ya mwaka uliopita pamoja na kuweka mikakati ya miezi 12 ijayo. 

Amesema mikakati hiyo inalenga kuboresha mazingira ya biashara, kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Amefafanua  kuwa TRA pia imefanya uchambuzi wa maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kilele cha Tuzo za Rais za Walipakodi, pamoja na maelekezo ya Rais wa Zanzibar yaliyotolewa katika kikao cha Baraza la Mapinduzi, ili kuhakikisha yanatekelezwa ipasavyo.

Kamishna Mkuu amewapongeza watumishi wa TRA kwa utendaji mzuri uliowezesha mamlaka hiyo kuendelea kuvunja rekodi za ukusanyaji wa mapato,huku  akibainisha kuwa watumishi na ofisi zilizofanya vizuri zaidi zitaendelea kutambuliwa na kupewa tuzo kama sehemu ya kuhamasisha utendaji wenye matokeo.

Aidha, amesema licha ya lengo hilo kuwa kubwa, linawezekana kufikiwa kutokana na rekodi nzuri ya ukusanyaji iliyojengwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, pamoja na ushirikiano unaoendelea kati ya viongozi na watumishi wa TRA.

Kamishna Mkuu amesisitiza kuwa TRA itaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais kwa kuimarisha ushirikiano na walipakodi, kurahisisha huduma za kodi, kuongeza wigo wa walipakodi (tax base) na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa sheria TRA kwa niaba   Naibu Kamishna Mkuu wa TRA ,Elisha Shigela  amesema kuwa ,Ushirikiano na Uzingatiaji wa Maadili unatakiwa  kuimarishwa ili kufikia malengo ya taasisi.
Aidha amewataka Watumishi wa taasisi  kuendelea kushirikiana na kutekeleza kwa vitendo maelekezo yanayotolewa na viongozi wao ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa ufanisi na kuendeleza rekodi nzuri ya utendaji.
Aidha amefafanua  kuwa ,mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kilichopita yametokana na mshikamano, ushirikiano na kujituma kwa watumishi wote huku ikisisitizwa kuwa ari hiyo inapaswa kuendelezwa ili kufanikisha malengo ya mwaka huu.
“Nawakumbusha watumishi  kuendelea kuzingatia misingi ya taasisi ikiwemo weledi, uwajibikaji, uadilifu na uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, huku ikielezwa kuwa maadili hayo ndiyo msingi wa utoaji wa huduma bora na mafanikio ya taasisi.”amesema