Na Jackline Minja, WMJJWM Ludewa, Njombe
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka wananchi wa Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe kushiriki kikamilifu katika kuibua, kujenga na kuendeleza miradi ya maendeleo katika kata zao ili kuharakisha maendeleo ya jamii na kutimiza Dira ya Taifa ya kujenga uchumi imara na ustawi wa wananchi.
Akizungumza katika nyakati tofauti tarehe 11 Julai, 2026 wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo katika Kata ya Masasi, Mhe. Mahundi amesema maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana kwa Serikali pekee bali yanahitaji ushiriki wa wananchi, sekta binafsi na wadau mbalimbali wenye moyo wa kuchangia maendeleo ya maeneo yao.
“Wananchi wanapaswa kuendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa ndiyo msingi wa kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa jamii. Ushirikiano huu unasaidia kuijenga Tanzania yenye maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho” amesema Naibu Waziri Mahundi.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuthamini na kuunga mkono watu binafsi na taasisi zinazochangia maendeleo ya jamii kupitia ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, usalama na huduma nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mhe. Olivanus Thomas amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wanaojitolea kuchangia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanailinda na kuitunza miradi hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Mhe. Joseph Kamonga, amemshukuru Bw. Iman Haule kwa kujitolea kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Masasi kwani mchango huo umeongeza upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi na kutoa wito kwa wazawa wengine wa Masasi na Ludewa kwa ujumla kuwekeza nyumbani na kushiriki katika kuleta maendeleo ya maeneo yao.
Aidha, Mwezeshaji wa miradi hiyo, Iman Haule, amesema lengo la kuwekeza katika miradi ya maendeleo si kwa ajili ya kujinufaisha binafsi, bali ni kuwagusa na kuwainua wananchi wa Kijiji cha Kingole na Kata ya Masasi kwa ujumla kupitia upatikanaji wa huduma muhimu zinazochochea maendeleo ya jamii.
Amesema ameamua kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuwa anaamini ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya vijiji na kuboresha maisha ya wananchi.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mahundi alitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la zahanati ya kujifungulia akina mama katika Kijiji cha Kingole huku akikagua ujenzi wa Kanisa la Anglikana Masasi, pamoja na kutembelea, kukagua na kuweka jiwe la msingi katika Jengo la Kituo cha Polisi cha Kata ya Masasi. Miradi hiyo imejengwa kwa ufadhili wa Bw. Iman Haule kupitia KUAMBIANA INVESTMENT COMPANY LIMITED, ikiwa ni mchango wake katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya, usalama na maendeleo ya jamii.

