Na. Veronica Mwafisi-Tabora

Tarehe 11 Julai, 2026

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewaelekeza Waajiri katika Sekta ya Umma mkoani Tabora kufanyia kazi madai ya watumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.Akifanya kikao cha majumuisho na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Tabora leo tarehe 11 Julai, 2026 baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu katika mkoa huo, Mhe. Kikwete amesema katika mwaka huu wa fedha Waajiri washughulikie masuala yote ya kiutumishi ikiwemo kupanda madaraja, kulipa malimbikizo, kuwabadilisha kada wanaostahili pamoja na madai mengine.

Amesema Ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali ya watumishi kuhusiana na kutoshughulikiwa stahiki zao jambo ambalo limekuwa likishusha ari ya utendaji kazi na kushindwa kuwahudumia wananchi kikamilifu.

Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka wananchi wake wapate huduma bora, mwaka huu wa fedha tushughulikie changamoto zote za watumishi ili watoe huduma kwa furaha, amesisiza.

Kuna watumishi wana sifa ya kupandishwa madaraja, wengine kubadilishiwa kada na wengine wana madai yao mbalimbali. Ninaelekeza wote wanaostahili watekelezewe na kama kuna changamoto yoyote mnayokutana nayo katika utekelezaji wa hili mtuletee Ofisini tuone namna ya kulitatua, ameongeza

Aidha, amewataka Maafisa Rasilimaliwatu kutoa ushauri kwa Waajiri utakaosaidia kutatua changamoto za kiutumishi. 

Amesema changamoto za kiutumishi zikishindwa kutatuliwa basi wa kulaumiwa si mwingine bali ni Maafisa Rasilimaliwatu kwani wanayo nafasi kubwa ya kutoa ushauri mzuri kulingana na taaluma zao.

Mhe. Kikwete amewapongeza Viongozi na Watumishi wa Mkoa huo kwa ushirikiano mzuri baina ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi uliochangia utekelezaji mzuri wa majukumu ya miradi ya maendeleo.

 Tunatekeleza Ilani ya Chama kilichoko madarakani, niwapongeze kwa ushirikiano baina yenu, endeleeni kufanya kazi kwa pamoja kwani ndio msingi wa maendeleo ya taifa letu, ameongeza

Vile vile Waziri Kikwete ametoa wito kwa Viongozi na Watumishi wa Mkoa huo kuzungumza na wananchi ikiwemo vijana na kusikiliza changamoto zao badala ya kusubiria viongozi wengine kutoka maeneo ya mbali kuzungumza.

Amesema kujua changamoto za vijana hao kunasaidia kwani wengine unakuta wanahitaji kitu kidogo cha kujiendeleza kiuchumi na kumuepusha kuingia katika masuala yasiyo na maadili.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Bi. Upendo Wella amemshukuru Mhe. Kikwete kwa ziara aliyoifanya katika mkoa huo ambayo itaenda kuboresha utendaji wa Watumishi kwa maendeleo ya taifa.