Mawaziri wa Nishati kutoka nchi wanachama wa Soko la Pamoja la Nishati Mashariki mwa Afrika (Eastern Africa Power Pool – EAPP) wameazimia kuharakisha utekelezaji wa soko la pamoja la umeme ili kuimarisha upatikanaji wa nishati, kuongeza biashara ya umeme kati ya nchi wanachama na kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa umeme katika ukanda huo.
Azimio hilo limefikiwa wakati wa Mkutano wa 22 wa Baraza la Mawaziri wa EAPP uliofanyika Julai 9 hadi 10, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo Tanzania iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Nishati.
Mkutano huo uliwakutanisha Mawaziri wa Nishati, wakuu wa taasisi za umeme na wawakilishi wa sekta ya nishati kutoka nchi wanachama wa EAPP kujadili hatua za kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia biashara ya umeme, uunganishaji wa gridi za taifa na matumizi bora ya rasilimali za nishati.
Maazimio yaliyofikiwa yanatarajiwa kuweka mfumo madhubuti utakaowezesha nchi wanachama kuuziana umeme kwa ufanisi, kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa nishati, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuvutia uwekezaji na kuimarisha maendeleo ya kijamii katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Mhe. Salome Makamba amesema maazimio hayo yatachangia kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme, kupunguza changamoto za upungufu na kukatika kwa umeme katika nchi wanachama, pamoja na kuimarisha ushindani na ufanisi wa taasisi za umeme kupitia kubadilishana uzoefu na teknolojia.
Amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika utaongeza kasi ya ukuaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, hali itakayochochea uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuzalisha ajira zaidi kwa vijana, ikiwemo kuwapa Watanzania fursa za kushiriki katika shughuli mbalimbali za kitaalamu ndani ya EAPP.
Akihitimisha mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAPP ambaye pia ni Waziri wa Maji na Nishati wa Ethiopia, Mhe. Dkt. Habtamu Itefa, amesema ushirikiano na mshikamano wa kikanda ni msingi muhimu katika kufanikisha uunganishaji wa mifumo ya umeme na kuhakikisha wananchi wa nchi wanachama wanapata huduma ya umeme salama, ya uhakika na endelevu.

