Happy Lazaro,Arusha .

Arusha .Jiji la Arusha limeendelea kuandika historia kwa kuvunja rekodi ya usajili wa Vikundi vya Ununuzi wa Umma (PPRA) nchini, hatua inayodhihirisha dhamira ya Halmashauri ya Jiji la Arusha katika kuwawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika fursa za zabuni za Serikali.

 Licha ya Serikali kuweka lengo kwa kila halmashauri kusajili angalau vikundi 150, Jiji la Arusha limevuka lengo hilo kwa kusajili jumla ya vikundi 306 na kutoa zabuni zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.3, hatua iliyoweka rekodi mpya ya utekelezaji nchini.  

Akipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli hiyo wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa mafanikio hayo makubwa, akisema yameonesha usimamizi madhubuti na utekelezaji wenye tija wa maelekezo ya Serikali katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia ushiriki wao kwenye ununuzi wa umma.  

Mwang’onda amesema mafanikio hayo yanaakisi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wa makundi yote wanapata fursa sawa za kushiriki katika uchumi na kunufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali. 

Ameutaka uongozi wa Jiji la Arusha kuendelea kusimamia uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi ili mafanikio hayo yaendelee kuimarisha maendeleo ya jiji na taifa kwa ujumla.