Tanzania imepata heshima ya kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya WSIS Prizes 2026 kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano ulioongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na ambayo hayakuwa na huduma ya mawasiliano nchini.

Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki(Mb.) katika hafla iliyofanyika Geneva, Uswisi, ikiwa ni utambuzi wa mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano. Mradi huo ulizinduliwa rasmi na Mhe. Rais tarehe 10 Aprili, 2026.

Mbali na kutwaa tuzo hiyo, Tanzania ilipata uteuzi katika vipengele saba (7) vya Tuzo za WSIS 2026 na kufanikiwa kuibuka na tuzo mbili kwa ujumla, huku pia ikitunukiwa vyeti vya kutambua miradi iliyofanya vizuri.