
Wananchi wakiwa katika banda la Kampuni ya ETDCO wakipewa taarifa za utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya umeme katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
…………..
Wananchi wameipongeza Kampuni ya ETDCO kwa utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya umeme kwa ufanisi, ubora na kuzingatia viwango vinavyohitajika.
Wakizungumza leo Julia 8, 2026 wakati waliotembelea banda la Kampuni ya ETDCO katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, wamesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umeimarisha huduma za umeme na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Mmoja wa wananchi hao, Samweli John, amesema kuwa ETDCO imeonyesha uwezo kwa kuhakikisha miradi yake inakamilika kwa ubora, ndani ya muda uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.
Naye Fatuma Hamasi amesema banda la ETDCO limemwezesha kupata uelewa wa kina kuhusu majukumu na miradi inayotekelezwa na kampuni hiyo, huku akieleza miradi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwafikishia wananchi huduma bora ya umeme.
Wametoa wito kwa ETDCO kuendelea kudumisha viwango vya ubora katika utekelezaji wa miradi yake, wakisisitiza kuwa maendeleo ya miundombinu ya umeme yana nafasi ya kukuza uchumi wa taifa.
Kwa sasa, ETDCO inatekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 132 yenye urefu wa kilometa 280 kutoka Tabora hadi Kigoma, wenye thamani ya shilingi bilioni 93.
Aidha, kampuni hiyo inatarajia kuanza kutekeleza mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wa kuunganisha umeme katika vitongoji vya mikoa ya Ruvuma na Katavi.
Maonesho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ni Fahari ya Tanzania,” sambamba na maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo.
