……………
SERIKALI kupitia Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi(VETA)na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), imezindua mradi wa Dumisha Amani unaohusisha vijana 60 kutoka wilaya tatu za mkoa wa Ruvuma wenye lengo la kuimarisha amani kwa maendeleo endelevu Tanzania.
Akitoa taarifa ya mradi wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika chuo cha VETA wilayani Songea, Afisa mkuza mitaala mwandamizi wa Veta makao makuu Alphocina Mshana amesema, mradi huo unalenga kuwafikia vijana 240 waliohitimu kwenye vyuo vya VETA katika mikoa minne ya pembezoni Lindi,Mtwara,Ruvuma na Kigoma.
Amesema kuwa,mradi huo unafadhiliwa na Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Serikali kupitia Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi(Veta) na ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha amani,ustawi wa vijana na maendeleo endelevu nchini.
Aidha amesema,mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea maarifa wahitimu hao kwa kuwapatia stadi ya ujuzi,stadi za maisha na stadi za ujasiriamali ambazo zitawawezesha kwenda katika soko la ajira kwa kujiajiri wenyewe kwa kuwa watapata maarifa au kuajiri watu wengine.
“Tunambua kwamba wakiwa na kipato,wataweza kustahimili misukosuko yoyote ambayo watakutananayo, kwa hiyo mradi huu umelenga kuwaangalia waliohitimu kwenye vyuo vya ufundi, lakini wako mtaani na hawajapata shughuli ya kujiingizia kipato japokuwa wamepata ujuzi”amesema Mshana.
Amesema,katika chuo cha Songea kuna wanafunzi wanaoendelea kupatiwa ujuzi na maarifa ambayo yatawawezesha kwenda kujiajiri au kuajiriwa ili waweze kupata kipato pamoja na kuwa mabalozi wazuri wa kudumisha amani kwa maendeleo endelevu hapa Tanzania.
Mkuu wa chuo cha Veta Songea Rahabu Mwakatundu ameekeza kuwa,mradi wa Dumisha Amani ni mradi wa kimkakati unaolenga kuwajengea wahitimu wa Veta maadili mema,utamaduni wa amani,uzalendo,mshikamano na stadi za maisha.
Mwakatundu amebainisha kuwa,kupitia mradi huo Serikali inamatumaini mkubwa kwamba vijana hao watakuwa raia wema na watachangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi wanapoingia katika soko la ajira au kujiajiri.
Amesema, katika utekelezaji wa mradi huo jumla ya wahitimu 60,wanawake 26 na wanaume 34 kutoka chuo cha Veta Songea wamechaguliwa na kuandaliwa kuwa mabalozi wa Amani katika jamii na wanatoka katika fani ya Ufundi Umeme wa majumbani, umeme wa magari,ushonaji,ufundi bomba na magari.
Kwa mujibu wa Mwakatundu,kupitia mafunzo hayo wahitimu watapenda kuwa mfano bora na kuishi kwa amani,kuhimiza mshikamano wa kijamii,kutatua migogoro kwa njia za amani na kutumia ufundi waliopata kujiletea maendeleo binafsi na ya Taifa.
Kwa upande wake Afisa miradi wa Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) Josephine Sepuka amesema,mradi huo unalenga kujenga daraja katika masuala ya amani na ufundi stadi na vijana watapata ujuzi utakaowasaidia katika safari yao ya maisha.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Songea Muhammadi Baggo,ameipongeza Serikali na UNDP kwa kutoa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia vijana waliohitimu kwenye chuo chua ufundi VETA,kuwa na maadili mema,kuwa wazalendo kwa nchi yao na kutambua umuhimu wa amani.
Baggo amesema,mradi wa Dumisha Amani kwa maendeleo endelevu Tanzania umekuja muda muafaka kwani unashirikisha moja kwa moja kundi muhimu la vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa na kupitia mradi huo Serikali itanufaika kupata vijana wengi wazalendo watakaotumika katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na ustawi wa nchi yetu.
Amewataka vijana,kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri za wilaya ili kupata mitaji kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuchumi badala ya kubaki wanalalamika.



