Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM – Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) imeibuka mshindi wa People Category Award katika Tuzo za Business SDG Awards 2026, ikiwa ni utambuzi wa juhudi zake za kuweka watu katika kitovu cha ukuaji endelevu kupitia uwekezaji unaowanufaisha wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara na jamii.

Tuzo hiyo, inayotolewa na Global Compact Network Tanzania, hutambua kampuni zinazochangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa vitendo, huku kipengele cha People kikitambua taasisi zinazoweka ustawi wa watu, ajira zenye staha na maendeleo jumuishi katika shughuli zao.

Ushindi wa TBL umetokana na mchango wake katika kuwawezesha wafanyakazi, wakulima wa malighafi, wauzaji wa rejareja, wasambazaji, wajasiriamali na jamii zinazozunguka shughuli zake, hatua inayodhihirisha dhamira ya kampuni ya kujenga biashara inayokua sambamba na maendeleo ya wananchi.

Kupitia programu mbalimbali za kilimo, TBL imeendelea kuwajengea uwezo wakulima kwa kuwapatia mafunzo, mbinu bora za uzalishaji, masoko na ushirikiano unaowawezesha kuongeza tija na kuendesha kilimo endelevu. Kampuni pia imeendelea kusaidia biashara ndogo na za kati kwa kutoa fursa zaidi kwa wadau wa mnyororo wake wa thamani kushiriki katika uchumi rasmi.

Ndani ya kampuni, TBL imeendelea kuimarisha mazingira salama ya kazi, ujumuishi, maadili na uwajibikaji, misingi ambayo imechangia kujenga uaminifu kwa wafanyakazi, washirika, wanahisa, wadhibiti na watumiaji wa bidhaa zake.

Akizungumzia ushindi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, alisema tuzo hiyo ni heshima kwa watu wote wanaochangia mafanikio ya kampuni na maendeleo ya jamii.

“Tuzo hii ni fahari kubwa kwa TBL kwa sababu inawatambua watu wanaofanikisha biashara yetu pamoja na jamii zinazohusiana na mnyororo wetu wa thamani. Wafanyakazi wetu, wakulima, wauzaji wa rejareja, wasambazaji, washirika na watumiaji wote wana mchango muhimu katika mafanikio yetu. Tunaendelea kukuza biashara kwa namna inayozalisha thamani halisi kwa Tanzania na kuchangia mustakabali jumuishi na endelevu zaidi,” alisema Kilpin.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, tuzo hiyo inaongeza historia ya TBL ya kutambuliwa kwa juhudi zake za uendelevu, ikiwemo usimamizi endelevu wa rasilimali za maji, matumizi ya vifungashio vinavyoweza kurejeshwa, urejelezaji wa mabaki ya uzalishaji na matumizi bora ya rasilimali.

TBL imesema ushindi wa People Category Award unaonyesha kuwa ajenda yake ya uendelevu haiishii kwenye utunzaji wa mazingira pekee, bali pia inalenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuunda fursa za kiuchumi, kuongeza ujuzi na kujenga thamani ya pamoja kwa jamii.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa itaendelea kuwekeza katika mipango inayoweka watu mbele ili kuhakikisha ukuaji wa biashara yake unaendelea kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi pamoja na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa.