Taasisi ya BRIGHT yawasilisha mpango wa kuanzisha Kituo cha Umahiri wa Teknolojia ya Betri*
DODOMA – Wizara ya Madini imeanza hatua za mwanzo za kujadili uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri wa Madini Mkakati kitakacholenga kutoa mafunzo ya teknolojia ya kuongeza thamani kwa madini na uzalishaji wa bidhaa za kisasa, ikiwemo betri za magari ya umeme na vifaa vya kuhifadhi nishati.
Kituo hicho kilipendekezwa kuanzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Taasisi ya BRIGHT ya Chuo Kikuu cha North Carolina, Marekani, ambayo imewasilisha mpango wake mbele ya wataalamu kutoka Wizara ya Madini, vyuo vikuu, na taasisi mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo.
Ujio huo ulirahisishwa na Chama cha Biashara Tanzania-Marekani (TACCUS), kupitia Mkatibu wa Bodi, Bi. Ronda Pierce, ambaye ameongoza ujumbe huo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kielimu na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Augustine Olall, aliipongeza Taasisi ya BRIGHT kwa kuonesha dhamira ya kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu na teknolojia ya uchakataji wa madini mkakati nchini Tanzania.
“Nia ya kuanzisha Kituo cha Umahiri nchini ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea kuongeza thamani ya madini yetu. Hatutaki tu kuzalisha madini, bali pia kuwa na uwezo wa kutengeneza bidhaa za mwisho zinazotokana na madini hayo,” alisema Olall.
Aliwataka wataalamu kutoka Wizara ya Madini pamoja na vyuo vikuu kushirikiana kwa karibu na taasisi hiyo na kusikiliza kwa makini mawasilisho yaliyotolewa ili kuhakikisha mpango huo unatekelezeka na kuwanufaisha Watanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Moses Kongola, alisema ujio wa Taasisi ya BRIGHT umefika wakati ambapo Tanzania inaelekeza nguvu kubwa katika kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi.
“Tanzania imeweka mkazo kwenye uchakataji na uongezaji thamani wa madini. Kituo hiki kitasaidia kujenga ujuzi wa kitaalamu na kuongeza uwezo wa nchi kuingia katika mnyororo wa thamani wa teknolojia za kisasa za nishati safi,” amesema Mhandisi Kongola.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika elimu, utafiti na teknolojia ni msingi muhimu wa kuhakikisha madini mkakati yanachangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akiwasilisha pendekezo la Taasisi ya BRIGHT, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Profesa Hemali Rathnayake, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye utajiri mkubwa wa madini mkakati yanayotumika kutengeneza betri za magari ya umeme na vifaa vya kuhifadhi nishati.
Alitaja madini hayo kuwa ni pamoja na Lithium, Kobalti, Nikeli, Kinywe (Graphite) na Rare Earth Elements.
“Changamoto kubwa siyo upatikanaji wa malighafi, bali ni ukosefu wa ujuzi, elimu na teknolojia ya kuzalisha bidhaa za mwisho. Taasisi ya BRIGHT imekuja na mpango wa kusaidia kuziba pengo hilo kupitia mafunzo kwa wanafunzi na wakufunzi wa vyuo vya Tanzania,” amesema Profesa Rathnayake.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za elimu ya juu unaweza kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa teknolojia za betri katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kikao hicho kilichofanyika Dodoma Julai 6, 2026 kimewakutanisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika na sekta ya madini na elimu ya juu, ikiwemo:
· Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) – Shule ya Madini na Jiolojia
· Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
· Chuo cha Madini Dodoma
· Chuo cha Madini Shinyanga (ESIS)
· Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
· Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) na
· Eyes Of Africa Refinery
Washiriki walijadili namna ya kuandaa mitaala ya pamoja, programu za mafunzo ya vitendo, na ushirikiano wa utafiti utakaowezesha Tanzania kunufaika zaidi na rasilimali zake za madini mkakati.
Iwapo mpango huo utafanikiwa, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye uwezo wa kutoa mafunzo maalumu ya teknolojia ya utengenezaji wa betri na bidhaa nyingine za nishati safi.
Wataalamu wanaamini kuwa hatua hiyo itaongeza ajira kwa vijana, kuvutia uwekezaji wa teknolojia ya juu, na kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika soko la kimataifa la betri za magari ya umeme.
Kwa sasa, Wizara ya Madini inaendelea kufanya tathmini ya mapendekezo yaliyowasilishwa ili kuweka msingi wa ushirikiano utakaoweza kuanzisha rasmi Kituo cha Umahiri wa Madini Mkakati Tanzania katika siku zijazo.

