Na.Sophia Kingimali.

CHUO cha Uhasibu Tanzania (TIA) kimewahimiza wanafunzi wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu pamoja na waajiri kutumia fursa zinazotolewa na chuo hicho, huku kikieleza kuwa kinaendelea kupanua huduma zake za elimu na mafunzo ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Akizungumza baada ya kutembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mwenyekiti wa bodi ya ushauri TIA Profesa Johavanes Aikael amesema TIA imejipanga vyema katika maonesho hayo kwa kuonyesha programu mbalimbali zinazotolewa, zikiwemo za uhasibu, manunuzi ya umma na taaluma nyingine za kitaaluma.

“Maonesho ya mwaka huu yamekuwa na ubora mkubwa zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita, jambo linalodhihirisha maendeleo ya sekta ya biashara, elimu na ubunifu nchini, hivyo tutarajie kuona maonesho yajayo yakizidi kuwa makubwa zaidi”,Amesema Prof.Aikael.

Ameongeza kuwa TIA inaendelea kupanuka kwa kasi kwa kuongeza uwezo wa kutoa elimu bora, hivyo amewakaribisha wanafunzi wapya kujiunga na kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo ili kujenga taifa lenye wataalamu wenye weledi.

Sambamba na hayo Prof Aikael ametoa rai kwa waajiri kushirikiana na chuo hicho kwa kupokea wanafunzi wanaokwenda mafunzo kwa vitendo (field), akieleza kuwa ushirikiano huo unawajengea wahitimu uzoefu unaowawezesha kuingia kwa urahisi katika soko la ajira.

Vilevile amewaomba wadau na wafadhili wa masomo kuendelea kusaidia vijana kupata elimu, akisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi muhimu wa kuandaa rasilimali watu itakayochochea maendeleo ya Taifa na kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi.