Na Mwandishi wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Joyce Komba, amesema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia maboresho ya mitaala, utoaji wa elimu jumuishi na uandaaji wa vitabu vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi wote.

Akizungumza katika banda la TET kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, wilayani Temeke Julai 6, 2026, Dkt. Komba alisema maboresho ya mitaala yanayotekelezwa na taasisi hiyo yanasisitiza elimu inayomfikia kila mtoto bila ubaguzi.

Alisema juhudi hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga rasilimali watu wenye maarifa, ujuzi na maadili, huku TET ikiwa na jukumu la kubuni na kuendeleza mitaala inayozingatia ujuzi, sayansi, teknolojia, ubunifu na matumizi ya TEHAMA ili kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika uchumi wa kisasa.

“Katika maboresho ya mitaala tunasisitiza sana elimu jumuishi ili kuhakikisha kila mtoto, ikiwemo mwenye mahitaji maalum, anapata haki yake ya msingi ya elimu,” alisema Dkt. Komba.

Alifafanua kuwa TET imeandaa vitabu vya maandishi ya Braille kwa wanafunzi wasioona pamoja na vitabu vyenye maandishi makubwa kwa wanafunzi wenye uoni hafifu ili kuwawezesha kujifunza kwa usawa na wanafunzi wengine.

Aidha, alisema taasisi hiyo imeandaa miongozo maalumu ya kuwasaidia walimu kufundisha watoto wenye mahitaji maalum, hususan wasioona, katika kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).

Dkt. Komba alisema hatua hiyo inaunga mkono Mkakati wa Kitaifa wa Kuimarisha Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anakuwa amemudu stadi hizo kabla ya kuhitimu darasa la tatu.

Kuhusu vitabu vya kiada, alisema TET inaendelea kutekeleza sera ya vitabu inayotaka kuwepo kitabu kimoja cha kiada na vitabu vingi vya ziada, huku ikiendelea kutoa elimu kwa wazazi na wadau kuhusu umuhimu wa kuwapatia watoto vitabu hivyo.

Aliongeza kuwa katika Maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu, TET imetoa punguzo maalumu la asilimia 10 kwa vitabu vya kiada vya mtaala ulioboreshwa na kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la taasisi hiyo ili kujipatia vitabu pamoja na huduma mbalimbali za elimu.