Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Mawaziri wa Kijamii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaohusisha sekta za Jinsia, Watoto, Vijana, Hifadhi ya Jamii, Kazi, na Uhamiaji unaendelea jijini Dar es Salaam, ambapo unafanyika kuanzia tarehe 2 hadi 7 Julai 2026, ukiwa na lengo la kuimarisha mtangamano na ustawi wa wananchi wa ukanda huo.
Mkutano huo umeanza na ngazi ya Wataalamu kuanzia tarehe 2 hadi 4 Julai, 2026 na utafuatiwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu kabla ya kuhitimishwa na Mkutano mkuu wa Mawaziri utakaofanyika tarehe 7 Julai, 2026.
Lengo kuu la mkutano ni kuandaa mikakati na sera zitakazosaidia kunufaisha makundi yote ya kijamii yakiwemo ya wanawake, vijana, watoto, wazee na watu wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha faida za mtangamano wa kiuchumi na kijamii wa EAC zinawafikia wote kwa usawa.
Maamuzi na maazimio yatakayopitishwa katika mkutano huu yanatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta za ajira, ulinzi wa jamii, na usimamizi wa masuala ya uhamiaji kikanda.

