Na Amos Charles, WAF – Dodoma
Wanafunzi wa maabara nchini wametakiwa kuongeza bidii katika masomo na mafunzo ya vitendo ili kuimarisha ufaulu katika mitihani ya usajili na kujenga umahiri unaohitajika katika utoaji wa huduma za maabara za afya kwa kufikia vigezo vilivyowekwa na Wizara.
Wito huo umetolewa leo Julai 3, 2026, jijini Dodoma na Kaimu Msajili wa Baraza la Wataalamu wa Maabara za Afya kutoka Wizara ya Afya Bi. Zubeda Salum, wakati akitangaza rasmi matokeo ya mtihani wa usajili uliofanyika kuanzia Machi 17 hadi Aprili 1, 2026.
“Jumla ya watahiniwa mia 714 walifanya mtihani huo, ambapo watahiniwa mia 366, sawa na asilimia 51 walifaulu huku watahiniwa mia 348 sawa na asilimia 49, wakishindwa kufikia kiwango cha ufaulu kilichowekwa na Wizara,” amesema Bi. Zubeda
Bi. Zubeda amesema matokeo hayo yanatoa angalizo kwa wanafunzi waliopo vyuoni kuongeza juhudi katika kujifunza kwa nadharia na vitendo ili kuongeza umahiri wa kitaaluma.
Aidha, Bi. Zubeda amewataka wakufunzi na wahadhiri kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mitaala inayotumika ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na uwezo unaokusudiwa katika sekta ya maabara.
“Watahiniwa waliofaulu wanapaswa kuendelea na hatua za kuomba usajili wa kudumu kupitia mfumo wa Health Practitioner Registration System (HPRS), huku wale ambao hawakufaulu wanatakiwa kujiandaa kwa mtihani wa marudio utakaotangazwa na Baraza,” amesema Bi. Zubeds
Amesema, Matokeo ya mtihani huo yanapatikana kupitia mfumo huo kwa kutumia jina la mtumiaji (username) na nenosiri (password) walilotumia wakati wa kuwasilisha maombi ya kufanya mtihani.
Baraza la Wataalamu wa Maabara za Afya lilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Sheria ya Wataalamu wa Maabara za Afya Na. 22 ya mwaka 2007, Sura ya 48, kwa lengo la kusimamia taaluma ya maabara za afya na kuhakikisha wataalamu wake wanafanya kazi kwa kuzingatia viwango na maadili ya taaluma likiwa na jukumu la kusajili, kuandikisha na kutoa leseni kwa wataalamu wenye sifa kwa mujibu wa sheria.

