Na John Walter -Babati, Manyara
Ubalozi wa Japan nchini Tanzania umeahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya elimu kwa kufadhili ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa na vyoo, ili kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Tanzania, Jin Hashimoto, wakati wa hafla ya kukabidhi mradi wa ujenzi wa madarasa matatu na matundu 29 ya vyoo katika Shule ya Msingi Orng’adida iliyopo Kata ya Qash, Wilaya ya Babati mkoani Manyara. Mradi huo umetekelezwa na Shirika la So They Can (STC) kwa ufadhili wa Ubalozi wa Japan nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la So They Can (STC), Roseylne Mariki, amesema mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 266, huku akibainisha kuwa kiasi kilichobaki cha takribani shilingi milioni 2.5 kimerejeshwa kwa Ubalozi wa Japan baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mradi.
Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, ameipongeza Serikali ya Japan kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kusaidia wananchi wa Tanzania kupitia miradi ya maendeleo.
Sillo amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa washirika wa maendeleo na wawekezaji, jambo linalowezesha utekelezaji wa miradi inayogusa maisha ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Mariam Muhaj, amesema msaada huo umeunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia, huku akiwakaribisha wadau wa maendeleo kuendelea kufikisha miradi kama hiyo katika maeneo mengine ya mkoa wa Manyara yenye uhitaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, John Noya, amesema mradi huo umepunguza mzigo wa michango kwa wananchi ambao hapo awali walilazimika kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule.
Wananchi wa Kata ya Qash wameishukuru Serikali ya Japan pamoja na Shirika la So They Can kwa kuwafikishia mradi huo, wakisema utasaidia kuboresha mazingira ya elimu na kuongeza ari ya wanafunzi na walimu katika mchakato wa kujifunza na kufundisha.

